HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 18, 2012

Under the Same Sun kugharamia matibabu ya mtoto Adam Robert

Mtoto Adam Robert akiwa amelazwa kwenye hospitali ya 
Wilaya ya Geita Mkoani Mwanza.
Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi linalofahamika kwa jina la Under the Same Sun limegharamia ticket za ndege ya za Mtoto Adam Robert, Mama yake Mzazi Sabina Saliboko na Daktari wake Dr. Patrick Bulugu ili kutokea Geita Mkoani Mwanza kuja Jijini Dar es Salaam ili kwenda hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Kitengo cha Tiba ya Mifupa – MOI kwa matibabu zaidi. 

Japokuwa majeraha ya Adam ambaye alidhuliwa na Baba yake kutoka na imani za kishirikina yameanza kupona kwa nje, bado anahitaji matibabu zaidi kwa mikono yake yote miwili. Adam hawezi kutumia mikono hiyo hivyo inamlazimu Mama yake Mzazi awe ana mlisha wakati wote.

Under The Same Sun waliombwa na Adam mwenyewe na pia Mama yake, Sabina Saliboko wakati Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo,Peter Ash alipomtembelea Adam katika Hospitali ya Wilaya ya Geita mwezi Novemba 2011, kumsaidia mtoto huyo kwa matibabu kabla ya kumpeleka shuleni. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari wake aliyempokea na anayemsindikiza hadi Muhimbili Dar es Salaam, Dr. Bulugu alisema kuwa mkono wa Adam wa kushoto uliposhambuliwa kwa panga, nerves ziliathirika na hivyo kuufanya mkono huo uwe kama umepooza.

Na hivyo wataalamu wa Muhimbili wataliangalia hilo na pia kumfundisha Adam jinsi ya kutumia vidole vyake viwili vilivyobakia katika mkono wake wa kulia ili avitumie kuandika na katika shughuli zingine zote zitakazomfanya aache kumtegemea Mama yake Mzazi kama vile kuoga, kuvaa na shughuli zingine.

Hivyo kutokana na hali hiyo Under The Same Sun wameamua kugharamia matibabu ya Adam katika kitengo cha Fast Track pale Muhimbili hadi hapo madaktari watakaporidhika na matibabu hayo. Na endapo Adam ataendelea na matibabu ya nje,Under The Same Sun watagharimia pia.

Under The Same Sun wamekuwa wakitoa misaada mbali mbali yenye gharama ya zaidi ya Shilingi Laki Nane ili kukidhi mahitaji ya Adam tangu alipolazwa kwenye hospitali ya Geita ikiwa ni pamoja na nguo, viatu, vyombo vya chakula na fedha zilizotolewa kwa Mama Adam tangu mtoto huyo aliposhambuliwa.

Fedha hizo pamoja na vitu vingine vingi ziliwawezesha kununua chakula kwa wakati wote walipokuwa Hospitali ya Wilaya ya Geita.

Kwa upande wa ushirikiano na TAS, UTSS wanashughulikia matibabu ya Adam na TAS wanashughulikia elimu ya Adam atakapomaliza matibabu yake na ndugu yake, Salum.

Kwa upande wa kaka yake Adam, Salum Robert, Chama cha Albino Tanzania – TAS kimesema kuwa kimepata shule jijini Dar es Salaam. Kwa hiyo gharama za kumsafirisha Salum zitatolewa na TAS.

Tunatoa wito kwa mashirika mengine katika jamii kushirikiana katika masuala kama haya na mengine mengi katika kuwasaidia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi. Na hasa katika kuondokana na imani na mila potofu zinazochangia ukatili wa kila aina dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad