Ali Choki |
Na Rachel Mwilligwa, Dar es Salaam
KATIKA kuhakikisha
inafurahia vema Siku Kuu ya Idd El Hadji na mashabiki wake, bendi ya Extra Bongo
wana Next Level au ukipenda unaweza kuwaita ‘Wazee wa Kizigo’, watatoa
burudani ya nguvu katika ukumbi wa Vatican
Hotel uliopo Sinza jijini Dar es Salaam.
Shoo ya nguvu ya bendi
hiyo itatolewa katika ukumbi huo ikiwa ni baada ya kumalizika kwa shoo ya
bonanza la kila Jumapili katika uwanja wa TP uliopo Sinza darajani ambapo Extra
Bongo sambamba na Bantu Group hutoa burudani katika viwanja hivyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana kuhusiana na shoo hiyo, Mkurugenzi wa Extra Bongo,
Ally Chocky aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kupata burudani nzuri na
kufurahia Siku kuu hiyo ya Idd kutoka kwa bendi yao ya Extra Bongo.
“Tumepania kuwapa raha
mashabiki wetu watakaofika Vatican, tunajua wengi wao watakuwa ni watu wazima,
ndio sababu tumeamua ingawa ni Siku Kuu tungeweza kufanya shoo ya kiingilio
tangu mchana, sisi tutatoa burudani bure pale viwanja vya TP Sinza ili watoto
nao wapate raha na kuifurahia siku kuu hii.
“Lakini kwa
watakaokuja ukumbini, basi watafurahia Idd kwani tutatoa shoo kali tunazotamba
nazo sasa kama ile ya Mdudu, Kizigo, Vuvuzela na nyingine nyingi kwani Super
Nyamwela ambaye ni kiongozi wa shoo katika bendi amepania mno kuonyesha
mavituuuz siku hiyo sambamba na
wanenguaji kama Aisha Madinda, Otilia
na wengine, hivyo hii si ya kukosa njoo ujioneee mwenyewe,” alisema Chocky.
Hata hivyo Chocky
alisema katika kuhakikisha Siku Kuu hiyo inanoga, wameandaa kufanya shoo
sambamba na kundi zima la khanga moja ama baikoko ambao bado wanaendelea na
mzungumzo nao hivyo kudai kuwa shoo hiyo itakuwa ni ya kufa mtu.
No comments:
Post a Comment