Msanii
maarufu wa Sanaa za Ufundi Gwalugano Ayoub (Kushoto) akiongea na wadau
wa Jukwaa la Sanaa wiki hii wakati akiwasilisha mada kuhusu Urithishwaji
wa Sanaa za Uchoraji kwa Watoto. Kulia ni Mratibu wa program ya Jukwaa
la Sanaa kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni
(CAJAtz),Hassan Bumbuli.
Mratibu
wa Programu ya Jukwaa la Sanaa kutoka CAJAtz,Hassan Bumbuli akisisitiza
jambo wakati akichokoza mjadala kwenye Jukwaa hilo. Kushoto ni Msanii
Gwalugano Ayoub.
Msanii wa Sanaa za maonyesho Mzee Kwama Bhallanga akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mada kwa umakini.
Na Mwandishi Wetu
Wadau
wa Sanaa wamesema kuwa umefika wakati wa mamlaka ya mapato nchini (TRA)
na shirika la viwango (TBS) kuingia kwenye sekta ya sanaa ili kuwe na
udhibiti wa mapato na ubora wa kazi za wasanii.
Wito
huo wameutoa kwa nyakati tofauti kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika
kila wiki kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo
walilia na uholela kwenye bidhaa na kazi za sanaa hali ambayo imekuwa
ikipoteza mapato ya wasanii na taifa kwa ujumla.
“Tatizo
kubwa limekuwa kwenye viwango vya kazi za wasanii,hapa kumekuwa na
mianya ya kuibiwa na wageni kutoka nje.Ni bahati mbaya kwamba hata
wanaponunua kazi zetu hawalipi kodi serikalini,hakuna udhibiti wa
forodha” alilalamika Ayoub Gwalugano ambaye ni Msanii wa sanaa za
uchoraji.
Alizidi
kueleza kwamba,wafanyabiashara kutoka nchi jirani wamekuwa wakinunua
kazi za wasanii wa Tanzania kisha kuzifanyia nakshi za mwisho
(finishing) na baadaye kuzigeuza za kuwa za kwao hali ambayo imekuwa
ikiwakosesha wasanii wa nyumbani haki miliki na mapato.
“Kazi
za wasanii zikiwa na nembo ya ubora si rahisi kuchukuliwa na mtu
mwingine. Wenzetu wa jirani wamekuwa wakinunua kazi zetu na kuzibadili
kidogo kisha kuziwekea nembo zao. Hii imekuwa ikiwafanya wasanii wetu
kuibiwa kazi zao” aliongeza Gwalugano.
Kuhusu
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wasanii wameiomba Serikali kuharakisha
utaratibu wa kudhibiti mapato katika tasnia hiyo kwani kumekuwa na wimbi
la wafanyabishara wanaojiingiza kwenye ununuzi wa kazi za sanaa hasa
kutoka nje pasipo kulipa kodi wala ushuru bandarini.
“Wageni
wamekuwa wakinunua michoro yetu kwa bei ndogo na kupita nayo kwenye
forodha bila kulipa kodi. Wengi wamekuwa wakidai kwamba wamebeba sampuli
(sample) lakini wanapofika kwao huiuza kwa bei kubwa” alieleza
Gwalugano.
Alimalizia
kwa kuishauri Serikali kupitia mamlaka hizi mbili kujikita katika
tasnia hii kwani kuna mapato mengi yanapotea ambayo si tu yanaweza
kuongeza pato la wasanii kwa kiwango kikubwa bali pia lile la Taifa.
No comments:
Post a Comment