Picha hii hapa ndio iliyosababisha hali hiyo...hata hivyo mbali na kumuamisha kuwa kulikuwa na vitisho na inadaiwa Wakubwa wa ngazi ya juu hawajashirikishwa juu ya hilo na walioamua ni wa ngazi ya chini..sasa..kweli TANZANIA tutafika??
Na Mwandishi Wetu.
KATIKA hali ya kutatanisha uongozi wa Jeshi la Polisi makao makuu jijini Dar seSalaam, umemhamisha mmoja wa askari wake, Koplo Chale Yunus kutoka Makao Makuuna kumpeleka katika Kikosi cha Mbwa na Farasi ambacho pia kipo jijini humo,ukimtuhumu kuvujisha taarifa kwenye vyombo vya habari kuhusu makazi yake.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo zimeeleza kuwa, baada ya habari ilizotolewa na moja ya magazeti ya habari hapa nchini, mwaka huu ikiwa na picha iliyoonyesha makazi ya askari huyo yaliyoko kwenye mahema eneo la Ukonga Magereza mkabala na Kanisa Katoliki, uongozi huo uliamua kumhoji na kufikia uamuzi wa kumhamisha kama adhabu.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya jeshi hilo makao makuu kimedokeza kwamba,askari huyo mwenye mke na watoto watatu alihamishwa siku mbili tu baada yahabari hizo kuandikwa gazetini na kuhojiwa na wakubwa wake.
Chanzo hicho kimebainisha kuwa maofisa wa polisi makao makuu walikerwa na habari hizo wakidai zimelidhalilisha jeshi hilo.
“Huyu bwana mnayemtafuta, amehamishwa tangu juzi, sasa hivi yuko kikosi cha Mbwa na Farasi, alituaga japo kuwa hakuweza kutueleza sababu ya kupewa uhamisho wa ghafla, lakini tunadhani ameadhibiwa maana awali alitudokeza kuwa aliitwa na bosi (hawakumtaja jina) ili ajieleze kwa tuhuma kwamba alikwenda kwenye vyombo vya habari kulalamikia makazi yake,” alieleza askari mmoja ambaye aliyekuwa akilinda Makao Makuu.
Hivi karibuni ripota wetu aligundua makazi ya polisi huyo na kubaini kuwa, mahema hayo yalikuwa ni makazi ya askari polisi anayefanyakazi Makao Makuu jijini Dares Salaam, kabla ya kufanya mahojiano na mkewe, Mariam Chale ambaye alielezakuwa, tangu nyumba waliyokuwa wakiishi kulipuliwa na mabomu ya jeshi kutokakambi ya Gongo la Mboto, wamekuwa wakiishi hapo mpaka sasa.
Jitihadaza kumpata Koplo Chale na uongozi wa jeshi hilo, ili kujua sababu za askari huyo kuendelea kuishi katika mahema ambayo hayana ubora, bado zinaendelea.
Akithibitisha kutokea kwa taflani hiyo, msemaji wa mkuu wa jeshi hilo, ASP Advera Senso alisema uhamisho wa askari huyo ulikuwa ni wa kawaida kwa kuwa ni mtaalam wa mbwa na dereva.
“Ni kweli nimethibitisha kuhamishwa kwa askari huyo, lakini ni jambo la kawaida tu,kwanza kwa sababu alikuwa ameazimwa kutoka huko kuletwa makao makuu, sasa amerudishwa alikotolewa wala halihusiani na suala la yeye kutoa taarifa za makazi yake kwenye gazeti, naomba ieleweke hivyo”, alibainisha msemaji huyo.
Alisema,jeshi la Polisi limekuwa likifanya jitihada za kuhakikisha askari wanapata makazi bora ikiwemo kuwajengea nyumba na hatimaye kuwaondoa katika makazi yanayoingiliana na raia, ili waweze kutenda kazi zao kwa ufanisi na kujenga nidhamu kazini.
Katika jitihada za kutafuta ukweli kuhusu sakata hilo, gazeti hili lilifanikiwa kumpata askari huyo kwa njia ya simu ya kiganjani, lakini alisita kuzungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa haruhusiwi kuzungumzia masuala yoyote ya jeshi hilo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na wahusika.
“Bwana mimi kweli naishi hapo na kweli nimehamishwa kutoka makao makuu, sasa niko katika kikosi cha mbwa na farasi, lakini nakuomba uwaone wahusika ndio watakupa maelezo zaidi, nafikiri ndugu mwandishi unajua utaratibu wa jeshi kutoa taarifa, wapo wanaohusika”, alisema askari huyo katika hali ya hofu.
Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani,Shamsi Vuai Nahodha ili kutolea ufafanuzi suala hilo,hazikufanikiwa kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment