Na Mwandishi Wetu,Dodoma
WAKATI mkoa maalum wa kimichezo wa Temeke ukiwa umejihakikishia kucheza robo fainali za taifa za mashindano ya mchezo wa pool yanayojulikana kama ‘Safari Lager National Championship 2011’, wenyeji wa fainali hizo mkoa wa Dodoma wenyewe umejiwekea mazingira magumu ya kusonga mbele baada ya kupoteza michezo yake yote miwili ya mwanzo.
Fainali za mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager, zinafanyikia kwenye ukumbi wa Kilimani Club mkoani hapa.
Mkoa wa Temeke umekuwa wa kwanza kujihakikishia kucheza hatua ya robo fainali kutoka kundi ‘A’ baada ya kushinda michezo yake mitatu dhidi ya Morogoro, Shinyanga na Arusha huku ikiwa imebakisha mchezo mmoja na Manyara.
Wenyeji wa fainali hizo mkoa wa Dodoma wenyewe umejiweka katika mazingira magumu ya kucheza hatua ya robo fainali baada ya kupoteza michezo yake miwili dhidi ya Ilala na Kilimanjaro huku ikiwa imebakisha michezo miwili dhidi ya Iringa na Mbeya katika kundi ‘B’.
Katika kundi ‘A’ mabingwa watetezi wa mashindano hayo , mkoa maalum wa Kinondoni umechelewa kujihakikishia kucheza robo fainali licha ya kushinda michezo yake miwili ya mwanzo dhidi ya Kagera na Mwanza lakini ilibidi Mwanza wapewe ushindi wa mezani kutokana na Kinondoni kuchelewa kuwakilisha fomu za usajili wa wachezaji wao.
Katika hali ambayo haikutegemewa Kinondoni wakiwa wanaongoza kwa magoli 13-3 dhidi ya Mwanza magoli ambayo tayari yalikuwa yamejihakikishia ushindi kwenye mchezo huo mara waliibuka viongozi wa Mwanza na kuanza kudai fomu za usajili wa wachezaji.
Kitendo cha Mwanza kudai fomu za usajili ambazo wakati huo Kinondoni hawakuwa nazo kutokana na mazoea ya miaka yote timu za mikoa kucheza fainali za taifa bila fomu za usajili wa wachezaji, kilipelekea mwenyekiti wa chama cha pool mkoa wa Dodoma ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa TAPA, Fredy Mushi kutoa ushindi kwa mkoa wa Mwanza.
Kinondoni licha ya kupoteza mchezo huo lakini bado una nafasi ya kusonga mbele endapo utashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya mkoa wa Tanga ambao nao tayari umeshinda mchezo mmoja dhidi ya Kagera.
Timu nane zitakazocheza robo fainali zitajulikana leo mara baada ya hatua ya makundi kukamilika ambapo Kundi ‘A’ na ‘B’ kila kundi linatoa timu tatu za kusonga mbele wakati kundi ‘C’ linatoa timu mbili.
Bingwa wa fainali hizo atajinyakulia fedha taslim Sh.milioni 5, mshindi wa pili Sh.milioni 3.5, mshindi wa tatu Sh. Milioni 2, na mshindi mshindi wan ne Sh.milioni 1.5.
No comments:
Post a Comment