HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 30, 2011

TAMASHA LA MTEMI MIRAMBO KUFANYIKA JULAI 8-10 MKOANI TABORA

  Mkurugenzi wa taasisi ya Chief Promotions,Amon Mkoga  (kulia) pamoja na Meneja wa Bia ya Balimi,Edith Bebwa wakionyesha moja ya matangazo ya Tamasha na Mtemi Mirambo.

TAMASHA la ngoma za utamaduni na maonyesho ya biashara la Mtemi Milambo linatarajiwa kurindima kuanzia Julai 8 hadi 10 kwenye Uwanja wa Chipukizi mjini Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa taasisi ya Chief Promotions ambao ndio waandaaji,Amon Mkoga, alisema kuwa tamasha hilo lina lengo la kuenzi na kuuendeleza utamaduni wa Kitanzania, hususani makabila makubwa ya mikoa ya Tabora, Shinyanga na Mwanza, ambao ni Wanyamwezi na Wasukuma.

Mkoga alisema pia michezo na maonyesho ya bidhaa zenye asili ya Kitanzania pia vitakuwepo,kama vile mchezo wa bao na kurusha mishale.

Alisema, Ijumaa ya Julai 8 shughuli itaanza saa 4:00 asubuhi hadi 12:00 jioni na kuendelea kwa muda huo huo hadi Jumapili Julai 10.

Mkurugenzi huyo alizitaja baadhi ya ngoma zitakazokuwemo wakati wa tamasha hilo kuwa ni pamoja na Manyanga, Maswezi, Uyeye, Bagalu, Bagika, Bazuba, Radu na nyinginezo.

Naye Meneja wa Bia ya Balimi, ambao ni kati ya wadhamini wa tamasha hilo,Bi Edith Bebwa, alisema wameamua kujitosa kudhamini tamasha hilo kwa mara ya pili ili kuwaenzi wateja wa bia hiyo ambayo ni mahususi kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

“Ngoma hizi za Wasukuma na Wanyamwezi huchezwa sana wakati wa mavuno, hivyo kwa kuwa Balimi ni bia ya mkulima tumeona tuungane kusherehea pamoja wakati wa mavuno huku tukienzi utamaduni wa Kitanzania,” alisema Bebwa.

Mgeni rasmi katika Tamasha hilo atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mheshimiwa Abeid Mwinyimusa.

Kauli mbiu ya Tamasha hili mwaka huu ni KUSHOKE KUKAYA yaani turudi nyumbani tafsiri ya Kiswahili toka kinyamwezi.

Mbali ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Balimi, wadhamini wengine ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ubalozi wa Switzerland ,Kalunde General Supplies, UNESCO na Fly 540(Shirika la ndege),Geita Goldmines, Magic Fm, Channel Ten na TBC.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad