HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 15, 2011

WAMACHINGA WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA USAFI WA MAZINGIRA


Na. Aron Msigwa - MAELEZO.

Serikali imewataka wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) kuepuka tabia ya kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa hali inayochangia uchafuzi wa mazingira katika miji mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira Dkt. Terezya Huvisa wakati akizungumza na wafanyabiashara (wamachinga) mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kukagua hali ya usafi wa mazingira katika Manispaa ya Songea.

Aidha alipowasili katika makutano ya barabara iendayo kwenye kituo kikuku cha polisi mjini Songea alishuhudia idadi kubwa ya wafanyabiashara (wamachinga) wakiwa wamepanga bidhaa chini na nyingine zikiwa juu ya meza kandokando mwa barabara hiyo hali iliyomlazimu kutoa agizo kwa viongozi wa manispaa hiyo kuhakikisha kuwa wanawaondoa wafanyabiashara hao na kuwapeleka katika maeneo halali waliyopangiwa.

Alisema serikali kupitia mamlaka za miji imejitahidi kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara wafanyabiashara hao lakini wengi wamekuwa wakikaidi maagizo ya serikali na kujiamulia kufanya biashara holela kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.

Aliwaambia wafanya biashara hao kuwa serikali haipingi na kamwe haitazuia biashara zao mahali popote nchini kama watazifanya kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi huku akionya uwezekano wa kutokea maafa endapo gari litakosea njia na kuingia eneo walipo.

"Nikweli vijana wengi mmekuwa na shauku ya kufanya biashara ndogondogo jambo ambalo serikali hatuna tatizo nalo, lakini hali hii ya kufanya biashara na kuchafua barabara za miji haikubaliki" Alisema Dkt. Huvisa huku akiwa amezungukwa na kundi la vijana hao.

Alibainisha kuwa katika uongozi wake suala la usafi na uhifadhi wa mazingira limepewa nafasi ya kwanza huku akiwataka wafanyabiashara hao mjini Songea kuelekea katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao yakiwemo maeneo ya Manzese, Bomba mbili na Soko kuu.

" Nasisitiza tena kwenye uongozi wangu sitaki uchafu, hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu hali hii tuliyonayo sisi, hivyo naomba wote waliopanga meza barabarani wazitoe kabla hazijachukuliwa na polisi" alisisitiza.

Naye Meya wa manispaa ya Songea Bw. Ally Manya alikiri kuwepo kwa hali hiyo ndani ya manispaa na kueleza kuwa tayari manispaa yake imeshatenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara hao lakini wengi wao wamekuwa wakiyakwepa maeneo hayo kwa kisingizio cha kukosa wateja.

Kwa upande wao wafanyabiashara katika maeneo hayo walikiri kuonyeshwa maeneo ya kufanyia biashara huku wakihoji uhalali wa viongozi wa manispaa hiyo kuwataka waondoke katika maeneo hayo wakati manispaa imekuwa ikiwatoza kodi ya shilingi 200 na miatano kila siku wanapopanga bidhaa zao.

“ Haiwezekani viongozi wa manispaa ya Songea leo watugeuke na kutuondoa, hili eneo linatambulika na ndio maana wanatutoza ushuru wa shilingi 200 na kutupatia risiti kila siku” Alibainisha mmoja wa wafanyabiashara hao Bw. Likanyangwa Tindwa.

Aidha wafanyabiashara hao walimuomba Mkurugenzi wa manispaa hiyo Bw. Nachoa Zacharia aliyekuwepo katika eneo hilo kuwatengea maeneo zaidi ya kufanyia biashara na kuboresha miundombinu ya maeneo yaliyopo sasa ili waweze kupata wateja kwa urahisi zaidi na kuepuka mivutano isiyo ya lazima.

1 comment:

  1. Mdogo wangu, umezungumzia mazingira na usafi, sasa mimi nilichoona ni kwamba vituo rasmi vya mabasi havipo tena maana nivituo vya biashara vimeshapata baraka zote, serikali, wanahabari na kila mtu mhusika hata wapanda mabasi. Vituo vyote ni sehemu rasmi ya biashara, basi na dalada ziendelee kusimaa katikati ya bara bara na wapanda mabasi wayakimbilie huko huko barabarani wakati magari nyuma yafunge foleni... jamani watanzania tupeane pole maana hatuambiwa maana, tumekwisha... labda tuandaliwe semina jinsi ya kutumia barabara, stendi ya basi, jinsi ya kuepuka foleni, namna ya kuheshimu wenzio.. nakadhalika ....

    ReplyDelete

Post Bottom Ad