HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 16, 2008

Msafara Wa Rais Kikwete Watupiwa Mawe Mkoani Mbeya

Msafara wa JK wapigwa mawe

Ziara ya Rais Jakaya Kikwete mkoani Mbeya imeingia dosari baada ya wananchi wa kijiji cha Kanga wilayani Chunya kupiga mawe magari sita yaliyokuwa katika msafara wake yakiwa yamewabeba mawaziri, waandishi wa habari na viongozi waandamizi wa serikali na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa. 

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika kijiji hicho majira ya saa 7:30 usiku wakati msafara wa Rais ukiwa njiani kuelekea Mbeya mjini ukitokea mji wa Mwakwajuni wilayani Chunya ambako Rais Kikwete alikuwa ziarani. 

Miongoni mwa magari yaliyopigwa mawe ni la Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawabwa, ambalo jiwe lilipiga upande wake na kugonga `wepa`. Hata hivyo, halikuvunja kioo wala kumjeruhi Waziri huyo. 

Magari mengine yaliyopigwa mawe ni la Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwatumu Mahiza, gari la Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Thomas Mwang`onda lenye namba za usajili T 894 AAY na gari namba STK 2429 lililokuwa limewabeba waandishi wa habari, ambalo limevunjwa vioo vya mlango na waandishi wawili kujeruhiwa. 

Magari mengine yaliyopigwa mawe na wananchi hao ni STK 3240 na STJ 3958 linalotumiwa na Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, katika msafara huo lilikuwa limewachukua maafisa wa serikali kutoka Ikulu.

Kutokana na tukio hilo, waandishi wawili wa magazeti ya serikali pamoja na kijana mmoja, Chipukizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wote walijeruhiwa na walipewa huduma ya kwanza na madaktari ambao wapo katika msafara wa Rais mara baada ya magari kuwasili katika Ikulu Ndogo ya mjini Mbeya majira ya saa 3.00 usiku. 

Baadhi ya viongozi waliozungumza na gazeti hili katika Ikulu Ndogo, walisema kuwa wananchi waliofanya tukio hilo walikuwa wamejipanga pembeni mwa barabara na baada ya magari manne ya mwanzo kupita, ndipo mawe yalianza kuvurumishwa. 

Baada ya magari hayo manne kupita, magari yaliyokuwa nyuma yalianza kuvurumishiwa mvua ya mawe na wananchi hao. 

Habari zaidi ambazo gazeti ilizipata zinaeleza kuwa hatua ya wananchi hao kufanya uhalifu huo ilitokana na hasira ya kushindwa kumwona Rais Kikwete baada ya kumsubiri kwa muda mrefu ili apite katika kijiji hicho na ili wamweleze kero zao. 

Kutokana na muda kuwa umekwenda na giza kutanda, Rais Kikwete hakuweza kusimama katika kijiji hicho, hali iliamsha hasira za watu hao ambao waliamua kukusanya mawe na kuanza kushambulia magari yaliyokuwa kwenye msafara. 

Hata hivyo, gari la Rais Kikwete, mke wake pamoja na walinzi wake hayakuhusika katika kadhia hiyo ya aina yake inayoashiria kuporomoka kwa maadili kwa kiwango cha juu kwa wananchi kiasi cha kutokuheshimu hata msafara wa kiongozi mkuu wa nchi. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, akizungumza na waandishi wa habari saa 3:30 usiku Ikulu Ndogo mjini hapa, alisema waliofanya kitendo hicho ni walevi na kwamba serikali itahakikisha inachukua hatua kali dhidi yao. Alisema kutokana na tukio hilo, ratiba ya Rais Kikwete katika ziara yake mkoani humo itabadilika na msafara wake hautatembea tena usiku. Kuanzia sasa hivi ratiba ya msafara wa Rais kutembelea sehemu mbalimbali za mkoa itabadilishwa kwa kuanza mapema asubuhi na kurejea mapema ili kuepuka tukio kama la leo (jana) lisijirudie, alisema. 

Mwakipesile alisema tayari kikosi cha Polisi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kimepelekwa katika kijiji cha Kanga kusaka wahusika wa tukio hilo la aibu kuwahi kutoka katika Jamhuri ya Tanzania. 
Tukio hili linatokea siku tano tu baada ya msafara wa Rais Kikwete kusimamishwa mara tatu na wakazi wa mkoa huo, Oktoba 10, mwaka huu siku alipoanza ziara ya siku 10. 
Katika matukio hayo yaliyoanzia Mbeya Mjini eneo la soko la Mwanjelwa, wananchi walisimama barabarani kuzuia msafara wake ili kumweleza kilio chao juu ya mafisadi kutokuadhibiwa na hali ya maisha kuzidi kuwa duni miongoni mwao. 
Pia walitaka kupewa sababu za kutokuwekwa matuta barabarani hali ambayo imesababisha watoto wao wengi kugongwa na magari; wananchi hao kadhalika walitaka kujua kwa nini hawana huduma ya maji safi.habari ni kwa msaada wa Thobias Mwanakatwe, ippmedia.

2 comments:

  1. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi. Rais wa nchi, amiri jeshi
    mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, mwenyekiti wa chama kinachotawala,
    mwenyekiti wa umoja wa afrika anapigwa mawe nyumbani kwake! Hii ni dalili
    mbaya.... Wananchi hawa wa Chunya nadhani wanatuma ujumbe kwa Rais Kikwete
    na Serikali yake.... Ukiacha mawaziri wachache waliowahi kuzomea na
    wananchi hili la kupiga mawe msafara wa amiri jeshi mkuu ni jipya....

    Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alisema kuwa ni walevi waliosubiri msafara wa Rais
    kwa muda mrefu na walikasirika baada ya msafara huo kuchelewa
    sana....Mbona miaka hiyo tulisubiri msafara wa viongozi kwa masaa na
    masaa, maduka yakiwa yamefungwa, shule zimefungwa na biashara zote, na
    watu kujipanga barabarani wakiwa na majani kumsubiri Rais apite... je
    walevi wapo Mbeya tu, wanakunywa pombe gani kali namna hiyo? Kwa tunaojua
    mlevi aliyekolea kinywaji hadi kutokuwa na subira, ataweza kweli kurusha
    jiwe?

    Mimi nadhani huu ni ujumbe kuwa wananchi wamesubiri maisha bora,
    wamesubiri ahadi lukuki na sasa wamechoka... Nadhani ni wakati wa Rais
    Kikwete na Serikali yake kujipanga upya.... Ile asilimia 80 iliyompa kura
    za ndiyo inaanza kupungua. au ni hao 20% waliompa kura za hapana ndiyo
    waliorusha mawe?

    Mkuu wa mkoa alinukuliwa katika gazeti la alasiri akisema kuwa suluhisho
    ni kuwa msafara wa Rais hautatembea tena usiku katika siku zilizobaki za
    ziara yake Mbeya... Suluhisho la ajabu kweli, katika hali ya kawaida hili
    ni suluhisho kweli? Rais awe na vizuizi vya kutembea katika nchi yake?

    Ni kweli sasa vyombo vya usalama vitamwagwa katka eneo husika na kuanza
    kutafuta hao walioitwa "walevi" na watu wengi watapata shida. mtego
    utakamata waliopo na wasiokuwepo...Lakini hilo si suluhisho. "walevi" wa
    aina hiyo tayari wapo wengi katka nchi yetu. hawa ni wale waliosubiri hali
    bora kwa muda mrefu bila kuiona. Hawa ni wale waliokata tamaa.... Huko
    Chunya ndo wameanza, lakini pengine si mwisho....

    Mungu atuepushe na hili balaa....

    ReplyDelete
  2. hii inaonyesha ni jinsi gani wanachi walivyochoka na maisha mabovu yaliyopo sasa hivi,maana waharibifu wa nchi wanajulikana lakini hawachukuliwi hatua sasa wanataka wananchi waendelee kumpenda kiongozi wao na wakati hafanyi kama wanavyotaka??

    ReplyDelete

Post Bottom Ad