kutoka ippmedia.com
Mkutano wa Sullivan: Mastaa Hatarini
2008-06-04
Na Aisha Hamza, PST - Arusha
Mastaa na vigogo wanaohudhuria mkutano wa nane wa Sullivan unaoendelea Jijini Arusha wamekuwa kivutio kikubwa na tayari imeelezwa kuwa sasa wako hatarini kunaswa na madada poa wanaojiuza, almaarufu kama `machangudoa` au kwa kifupi `ma-cd`.
Wakizungumza na mwandishi wa PST, madada hao ambao kiasi wamesabababisha bei za huduma zinazotolewa na saluni za kike Jijini hapa kuwa za juu maradufu, wamesema watahakikisha kuwa hawaondoki bure, pasi na kuwapata viongozi na wafanyabiashara zaidi ya 4,000 wanaohudhuria mkutano huo wa kihistoria, akiwemo mcheza filamu maarufu wa Kimarekani, Chriss Tucker.
Aidha, madada wengine waliomwagika Jijini hapa, mbali na Wabongo ambao wametoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Jiji la Dar, Mwanza, Tanga na kwingineko, pia wapo warembo toka katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na hata Ethiopia.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hii umebaini kuwa wengi wa ma-cd hao wamepania kuwang'oa mastaa waliopo hapa kwa nia ya kujipatia pesa na pia, kujipa umaarufu wa kuweza kutembea na watu wenye majina makubwa duniani.
``Nimepoteza fedha nyingi za nauli na gharama nyinginezo za kutoka kwetu Nairobi hadi hapa... siwezi kuondoka bila kumpata mazee (mpenzi) mwenye pesa za kunibadilishia maisha yangu," akasema mmoja wa madada hao kibao wanaoonekana wakiranda katika maeneo maarufu ya Jijini hapa.
Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya usalama wa wageni waliopo Jijini hapa na ambao wameonekana wakiwindwa kila kona na madada hao kibao wanaojiuza, Kamanda wa Polisi Jijini hapa, Basilio Matei, amesema hakuna hofu yoyote kwani wao wamejipanga vyema katika kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.
Akasema Kamanda Basilio kuwa hivi sasa, wao wanaendelea na hatua za kuimarisha ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwasweka ndani wadada wote wanaoonekana wakijipitisha bila shughuli maalum katika maeneo jirani na ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa AICC, ambako kunafanyikia mkutano huo wa Sullivan.
``...ila hatuwezi kuwakamata kwa sababu ya kudai kuwa wanajiuza, hapana... tunaweza kuwakamata wadada hao kwa kosa la uzururaji,`` akasema Kamanda Matei. ``Yawezekana wapo mahali hapo kwa nia ya kuuza miili yao, lakini sisi tutawakamata kwa kosa la uzururaji tu... na wakienda mahabusu wanaachiwa mara moja kwa kutoa faini,`` akasisitiza Kamanda Basilio.
Hata hivyo, ameahidi kuwatuma maaskari wake kwenda kuwakamata watu kama hao ili wasilete sifa mbaya kwa nchi yetu na kueleza kuwa watazidisha ulinzi katika maeneo yote wanayopenda kuwavizia watu maarufu.
Mbali na mastaa mbalimbali akiwemo mpigania haki za watu weusi Mchungaji Jesse Jackson, pia mkutano huo wa aina yake unahudhuriwa na marais kibao akiwemo mwenyeji wao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Nigeria Bwana Olusigen Obasanjo.
SOURCE: Alasiri
No comments:
Post a Comment