HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 14, 2026

NYONGO AITAKA MKURANGA KUHARAKISHA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI MBEZI GONGONI

 

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuhakikisha inasimamia na kuharakisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Mbezi Gongoni ili ikamilike kwa wakati na kuanza kupokea wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2027.

Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kukamilisha taratibu za usajili wa shule hiyo mapema ili kuwezesha kuanza kwa shughuli za utoaji wa elimu mara baada ya kukamilika kwa miundombinu inayohitajika.

Mhe. Nyongo ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo iliyopo katika Kijiji cha Msufini Kidete, Kata ya Mbezi, katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 16.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka Halmashauri kutenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabweni yatakayowawezesha wanafunzi wanaoishi mbali na shule hiyo kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia, pamoja na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.

“Ni vyema shule hii ikawa na mabweni ili kuwasaidia wanafunzi wanaoishi mbali kupata nafasi ya kuishi karibu na shule. Hivyo, nawaelekeza kuhakikisha mnatenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo,” amesema Nyongo.

Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Mkuranga kwa kutumia mapato ya ndani kutekeleza mradi huo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuelekeza rasilimali za Halmashauri katika miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan katika sekta ya elimu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Msufini Kidete, Beatrice Anthony Deref, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi ilianza Juni 2024 na kukamilika Juni 2026 kwa gharama ya Shilingi milioni 196.2 zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Awamu hiyo ilihusisha ujenzi wa vyumba sita vya madarasa, ofisi mbili na matundu 12 ya vyoo.

Amesema awamu ya pili iliyoanza Oktoba 2026 na inayotarajiwa kukamilika Januari 2027, inagharimu Shilingi milioni 426 kutoka mapato ya ndani na inahusisha ujenzi wa vyumba 15 vya madarasa, maabara moja na matundu 18 ya vyoo.

Ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuongeza nafasi za wanafunzi kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2027 na 2028, kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kupunguza adha ya wanafunzi wa Kata ya Mbezi ambao wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata elimu katika Shule za Sekondari Shungubweni na Kitumbo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad