Makamu wa Rais wa Kwanza Othman Masoud Othman akizungumza katika mkutano wa Maafisa Utumishi ulioendana na uzinduzi wa Mfumo wa Bima ya Maisha uliunganishwa Watumishi Portal
Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Insurance Kaimu Mkeyenge akimsikiliza Makamu wa Rais wa Kwanza Othman Masoud Othman katika mkutano wa Maafisa Utumishi ulioendana na uzinduzi wa Mfumo wa Bima ya Maisha uliunganishwa Watumishi Portal.
Maafisa utumimishi wakifatilia Mada ya Bima ya Maisha inayoyolewa na NIC Insurance
ZANZIBAR. Watumishi wa umma sasa wanaweza kujiunga na bima ya maisha ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) kupitia Watumishi Portal (ESS), mfumo wanaoutumia kupata huduma za kiutumishi. Kwa kuweka huduma hiyo kwenye mfumo huo, NIC inalenga kurahisisha usajili na kupunguza matumizi ya fomu za karatasi.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, alizindua huduma hiyo Jumanne, tarehe 10 Novemba 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMNet), uliofanyika Zanzibar. Othman pia alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Kaimu Abdi Mkeyenge, alisema huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika za kuwafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma katika taasisi za umma.
Katika mkakati wake wa matumizi ya teknolojia, NIC imeongeza njia ambazo mteja anaweza kutumia kupata taarifa, kununua bima na kufuatilia madai kupitia tovuti rasmi ya www.nicinsurance.co.tz, App ya NIC Kiganjani, na NIC Customer Portal. Shirika pia linatoa huduma kupitia NIC Rafiki kwenye WhatsApp.
Kupitia njia hizo, NIC inalenga kukidhi mahitaji ya wateja na kupanua upatikanaji wa ulinzi wa bima kwa watu binafsi, familia, taasisi na jamii kwa ujumla.
Kutoa huduma ya bima kupitia mfumo ambao watumishi tayari wanautumia kunaendana na Lengo la Nne la Dira 2050, linalohimiza matumizi ya teknolojia za kidigitali kuchochea ubunifu. Miongoni mwa shabaha za lengo hilo ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zinapatikana kupitia mifumo ya kidigitali iliyo salama na jumuishi.
Kwa mtumishi wa umma, urahisi wa kujiunga na bima ya maisha unatoa nafasi ya kupanga mapema ulinzi wa kifedha wa familia yake. Kwa kurahisisha hatua hiyo, NIC inalenga kuimarisha utamaduni wa kutumia bima kama sehemu ya mipango ya kifedha ya familia.


.jpeg)

No comments:
Post a Comment