HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 21, 2026

NGOs ZATAKIWA KUJITEGEMEA KIFEDHA, WAZIRI MKUU KUFUNGUA JUKWAA DODOMA

 


Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yametakiwa kubuni vyanzo vya ndani vya mapato na kuimarisha ubia na sekta binafsi ili kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje na kuhakikisha uendelevu wa shughuli zake za kijamii.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Jukwaa la Sita la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, litakalofanyika jijini Dodoma kuanzia Novemba 25 hadi 28, 2026.

Dkt. Gwajima amesema changamoto ya utegemezi wa wafadhili, masharti magumu ya upatikanaji wa fedha na kutotabirika kwa ufadhili ni miongoni mwa mambo yanayohitaji majadiliano ya kina ili kupata suluhisho litakalowezesha mashirika hayo kuendelea kutoa huduma kwa jamii.

Amesema kutokana na hali hiyo, jukwaa la mwaka huu limejikita katika kaulimbiu isemayo, “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”

Katika jukwaa hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, huku washiriki takribani 3,500 kutoka serikalini, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali wakitarajiwa kushiriki.

Dkt. Gwajima amesema zaidi ya mashirika 8,000 yaliyosajiliwa nchini yanatoa huduma katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, maji, kilimo, uhifadhi wa mazingira, uwezeshaji kiuchumi, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na ulinzi wa kijamii, hali inayodhihirisha umuhimu wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.

Amesema mchango wa mashirika hayo ni muhimu zaidi katika kipindi hiki ambacho Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyozinduliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025.

Ameeleza kuwa Wizara hiyo iliandaa Juni 2026 Mkakati wa Kitaifa wa Mageuzi ya Kijamii na Maendeleo ya Mtaji Watu katika kufikia malengo ya Dira 2050, unaojulikana kama Jamii Ajenda Dira 2050, unaoongozwa na falsafa ya “Familia Imara, Jamii Imara, Taifa Imara.”

Kwa mujibu wa Waziri huyo, jukwaa hilo ni la sita tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 na litatoa fursa kwa wadau kujadili mafanikio, changamoto na fursa za ufadhili, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuimarisha uendelevu wa mashirika hayo.

Amesema mijadala itafanyika Novemba 25 na 26 katika Ukumbi wa Urio Executive, huku kilele cha jukwaa kikifanyika Novemba 27 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Aidha, Novemba 28 kutakuwa na mbio za hisani katika Uwanja wa Jamhuri, utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Dodoma, shughuli za uwajibikaji kwa jamii pamoja na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazotekelezwa na mashirika na wadau wa sekta binafsi.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa taasisi za serikali, mamlaka za serikali za mitaa, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na wananchi kujitokeza kushiriki jukwaa hilo ili kuongeza maarifa na kujenga mikakati ya pamoja ya kuimarisha sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad