HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 12, 2026

MAKAMU WA RAIS AAGIZA UCHUNGUZI WA UFANISI WA VIUATILIFU VYA KOROSHO

 





MAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameanza ziara ya kikazi mkoani Mtwara tarehe 12 Novemba 2026, ambapo amekagua miradi mbalimbali na kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Masasi, Newala na Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Sekta ya Kilimo.

Katika mikutano hiyo ya hadhara, Makamu wa Rais amewahimiza wakulima wa zao la Korosho kuongeza uzalishaji ili kuinua kipato cha mkulima mmoja mmoja, kukuza uchumi wa mkoa wa Mtwara na kuongeza mchango wa zao hilo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa Serikali inatambua changamoto zilizojitokeza katika upatikanaji na matumizi ya viuatilifu vya Korosho (sulfur) msimu uliopita. Kutokana na hali hiyo, ameiagiza Wizara ya Kilimo kufanya tathmini na uchunguzi wa kina kubaini iwapo viuatilifu vilivyotumika vilikuwa vimechakachuliwa au havikuwa na ufanisi uliotarajiwa.

Amesisitiza kuwa endapo itabainika kuwa viuatilifu vya maji havina ufanisi unaohitajika, Wizara ichukue hatua stahiki, ikiwemo kuangalia uwezekano wa kurejesha matumizi ya viuatilifu vya unga ili kuhakikisha wakulima wanapata huduma bora ya kudhibiti visumbufu vya zao la Korosho na kulinda uzalishaji wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amesema kuwa tayari timu ya wataalamu imeundwa kufanya tathmini ya kiuatilifu aina ya ‘sulfur’ ili kubaini iwapo sulfur ya unga au maji ndiyo inayofaa zaidi kutumika katika msimu ujao wa uzalishaji wa zao la Korosho.

Aidha, amewapongeza wakulima wa Tandahimba na Newala kupitia Chama chao cha TANECU kwa kufanikisha mauzo ya zaidi ya tani 70,000 za Korosho tangu kuanza kwa msimu wa minada wa Mwaka 2026/2027.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad