Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
GHARAMA za matibabu ya magonjwa makubwa zinaweza kuzilazimisha familia kutumia akiba, kuuza mali na kutegemea michango ya ndugu na marafiki, hali inayodhihirisha umuhimu wa Bima ya Afya katika kulinda ustawi wa familia na uchumi wa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato Kosuri, amevitaka vyombo vya habari kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya na manufaa yake katika kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.
Kosuri amesema huduma za afya si suala la matibabu pekee, bali pia ni sehemu muhimu ya kulinda ustawi wa familia na uchumi wake, akibainisha kuwa ugonjwa unaohitaji matibabu ya gharama kubwa unaweza kuathiri hali ya kifedha ya familia ambayo haina maandalizi ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na OTR, Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam, amesema mifumo ya Bima ya Afya inasaidia kugawana hatari za gharama za matibabu na kupunguza mzigo unaoweza kuzikabili familia.
“Hali hii inaibua maswali muhimu kuhusu mustakabali wa familia ambazo hazina ndugu, marafiki au uwezo wa kifedha wa kuwasaidia zinapokabiliwa na magonjwa yanayohitaji matibabu ya gharama kubwa.
“Hapa ndipo umuhimu wa NHIF na mifumo ya Bima ya Afya unapopaswa kuonekana, kwa kuwa inasaidia kugawana hatari zinazotokana na gharama za matibabu na kupunguza mzigo kwa familia moja moja,” amesema Kosuri.
Amesema NHIF ina jukumu muhimu katika kulinda rasilimali watu na jamii kwa ujumla kwa kusaidia wananchi kupata huduma za afya zinazowawezesha kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuchangia ujenzi wa uchumi imara.
Ameongeza kuwa maendeleo ya taifa hayapaswi kupimwa kwa kuzingatia mitaji na miradi pekee, bali pia ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa jamii yenye afya njema ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yake kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na NHIF, haki na wajibu wa wanachama pamoja na namna ya kunufaika na huduma hizo.
Amesema ushirikiano kati ya taasisi za afya na vyombo vya habari, hususan wahariri na waandishi wa habari, unaweza kuongeza uelewa na hamasa ya wananchi kujiunga na mifumo ya Bima ya Afya na kufanya maamuzi sahihi kuhusu ulinzi wa afya zao na familia zao.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za OTR kuimarisha uwazi, utawala bora na uwajibikaji katika taasisi na mashirika ya umma kupitia majadiliano ya moja kwa moja na wahariri wa vyombo vya habari.
.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment