Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo ni fursa ya kutathmini mafanikio, hali ya sasa na mwelekeo wa baadaye katika kuchochea maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Nungu amesema COSTECH inajivunia kuendelea kuwepo kwa miaka 40, jambo linalodhihirisha umuhimu wake katika kuendeleza tafiti na ubunifu kwa manufaa ya Taifa.
Ameongeza kuwa mafanikio ya COSTECH yanachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inategemea sayansi na teknolojia kuboresha maisha ya Watanzania, kuongeza tija katika sekta za afya na kilimo, na kukuza uchumi.
Aidha, amesema Tanzania imepiga hatua katika kukuza utamaduni wa ubunifu, ambapo vijana na watafiti wamebuni bidhaa na huduma mbalimbali ambazo tayari zimeingia sokoni.
Katika maadhimisho hayo, COSTECH imeandaa mijadala kuhusu mustakabali wa sayansi, vipaumbele vya utafiti, ushirikiano wa kimataifa na nafasi ya sekta binafsi.
Dkt. Nungu amebainisha pia kuwa COSTECH inaendelea kuimarisha mfumo wa NIST, utakaosaidia upatikanaji wa taarifa na ripoti za utafiti kwa ajili ya kufanya maamuzi na kupanga vipaumbele vya maendeleo

No comments:
Post a Comment