Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Mhe.Cosato Chumi, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha mshikamano na biashara ya ndani ya kikanda ili kukabiliana na athari za migogoro ya kimataifa.
Chumi amesema migogoro inayoendelea duniani imeonesha umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kujenga uchumi imara katika sekta za nishati, kilimo, mbolea na biashara, akisisitiza kuwa soko la zaidi ya watu milioni 300 ndani ya EAC ni fursa kubwa ya kukuza nguvu ya kiuchumi ya ukanda huo.
Akizungumza katika Semina ya Mahusiano ya Mabunge kati ya Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Umoja wa Ulaya (Interparliamentary Relations Seminar), amesema nchi wanachama zinapaswa kuondoa vikwazo vya biashara, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika ukanda huo ili kupunguza utegemezi wa masoko ya nje.
Aidha, amesisitiza kuwa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kwa kushirikiana na mabunge ya kitaifa, lina wajibu wa kuweka na kusimamia sheria na mifumo inayolinda amani, usalama na ustawi wa kiuchumi wa wananchi.
Chumi amesema ushirikiano wa kikanda si jambo la hiari, bali ni hitaji la kimkakati katika kuimarisha usalama wa kiuchumi, kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Semina hiyo imejadili athari za migogoro ya kimataifa na mabadiliko ya mifumo ya biashara duniani, pamoja na mikakati ya mabunge katika kulinda usalama wa kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.


.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment