Na Mwandishi Wetu.
Benki ya CRDB imesaini makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya China (China Development Bank – CDB), yanayofungua fursa za ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati, uwekezaji na maendeleo ya sekta muhimu za uchumi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Ushirikiano huo pia unalenga kuimarisha biashara kati ya Tanzania na China, ambayo thamani yake inatarajiwa kuvuka Shilingi trilioni 31 mwaka 2026.
Makubaliano hayo yanafungua fursa za ufadhili katika sekta za nishati, madini, viwanda, biashara ndogo na za kati, pamoja na miradi ya maendeleo endelevu. Miongoni mwa miradi inayotazamwa kunufaika na fursa za ushirikiano huo ni ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi na Kuchakata Taarifa (Data Centre) Zanzibar na mradi wa kufufua na kuboresha Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa benki hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Prof. Neema Mori, ambaye ameeleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya Benki ya CRDB kama mshirika wa kimkakati katika maendeleo ya Taifa, hususan katika kuvutia mitaji ya kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa itakayochochea mageuzi ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema ushirikiano huo unafungua ukurasa mpya wa fursa za uwekezaji kwa kuunganisha mitaji ya kimataifa na mahitaji ya maendeleo nchini, huku ukitarajiwa kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha miundombinu na kukuza ushindani wa Tanzania katika biashara za kikanda na kimataifa, na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, Huang Zhiqiang, ameeleza kuwa ushirikiano huo unaimarisha uhusiano wa kifedha na kiuchumi kati ya Tanzania na China, huku ukifungua fursa za kuendeleza miradi yenye tija na uwekezaji wa muda mrefu utakaonufaisha wafanyabiashara na wananchi wa nchi zote mbili.

.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment