HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 17, 2026

TACAF Yawezesha Miradi 104 ya Lugha na Fasihi kwa Sh bilioni 2.3

 



Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Utamaduni na Sanaa (TACAF) umewezesha miradi 104 katika eneo la lugha na fasihi kwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 2.36, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza fasihi andishi, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza katika maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania na uzinduzi wa vitabu leo Oktoba 16, 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa TACAF, Nyakaho Mahemba, amesema uwezeshaji huo umechangia upatikanaji wa mashine za uchapishaji, uboreshaji wa miundombinu ya maduka ya vitabu pamoja na uchapishaji wa vitabu vinavyotumika mashuleni, maofisini, vyuoni na hotelini.

Amesema mfuko huo ulianzishwa kwa lengo la kuinua ubora wa kazi za utamaduni na sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara, kuzalisha ajira na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.

Mahemba amesema TACAF inahudumia maeneo mbalimbali ya sanaa, ikiwamo sanaa za maonyesho, sanaa za ufundi, filamu na muziki, huku upande wa utamaduni ukijikita katika lugha na fasihi, ikiwamo uandishi wa makala, miswada, vitabu, mashairi na ngonjera pamoja na uchapishaji.

Ameeleza kuwa fasihi andishi ina nafasi muhimu katika kuwasilisha mawazo, hisia, maarifa na uzoefu wa binadamu kupitia maandishi, huku ikisaidia kuhifadhi historia, mila, desturi, maadili na tamaduni za jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Aidha, amesema uandishi una mchango katika kuelimisha jamii, kuburudisha, kukosoa maovu na kuhamasisha mabadiliko chanya, hivyo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya lugha, fasihi na jamii kwa ujumla.

Mahemba ameongeza kuwa fasihi andishi ni msingi wa ubunifu katika sanaa nyingine, ikiwamo filamu, tamthiliya, muziki na sanaa za maonyesho, kupitia uandishi wa miswada inayotumika kuandaa kazi mbalimbali za kisanii.

Amesema kutokana na mchango huo, ni muhimu kuendelea kuwekeza katika uandishi, kuimarisha utamaduni wa kusoma, kukuza uchapishaji na kujenga ushirikiano kati ya fasihi andishi na sanaa nyingine ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuhifadhi urithi wa kitamaduni kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda, amewataka waandishi na wachapishaji wa vitabu kuendelea kuandaa machapisho yanayokidhi mahitaji ya sasa ya jamii, yakiwemo vitabu vya watoto, vitabu vya rejea, kamusi na machapisho yanayohifadhi historia na utamaduni wa Tanzania.

Amesema vitabu vina mchango mkubwa katika kuendeleza elimu, kuhifadhi maarifa na kukuza sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo utalii, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha uchapishaji na usomaji ili tasnia hiyo iweze kukua na kushindana kimataifa.

Amesema kamusi zina nafasi ya pekee katika kukuza Kiswahili, kuimarisha mawasiliano, kuhifadhi msamiati na kurahisisha upatikanaji wa maarifa katika elimu, sayansi, teknolojia, biashara, diplomasia na maeneo mengine ya maendeleo.

Ntonda amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa wanafunzi na vijana wa vyuo, akieleza kuwa juhudi za waandishi na wachapishaji zinapaswa kwenda sambamba na hamasa kwa jamii kutumia vitabu kujielimisha na kuongeza ujuzi.

Ameahidi kuwa wizara itayafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa na wadau wa uchapishaji wa vitabu, kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika, huku akihimiza kuwepo kwa mikakati ya kuendeleza maonyesho ya vitabu na kuongeza ushiriki wa wadau ili kukuza tasnia hiyo nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TACAF, Nyakaho Mahemba, Akizungumza katika maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania na uzinduzi wa vitabu leo Oktoba 16, 2026.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad