Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Seif Shekalaghe ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utoaji mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) ili taasisi hiyo iendelee kuzalisha wahitimu bora zaidi watakaosaidia taifa kwenye masuala mbalimbali ya kisheria.
Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo wakati akizungumza na menejimenti ya LST katika ziara yake ya kikazi alipotembelea taasisi hiyo leo tarehe 23 Oktoba, 2026 jijini Dar es Salaam.
"Nawapongeza kwa kutekeleza kwa ufanisi jukumu lenu la kuwanoa wanafunzi wetu wa sheria ambao wakihitimu mafunzo haya ya uanasheria kwa vitendo wanaenda kulisaidia taifa kwenye mambo mbalimbali hivyo nawaahidi Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana nanyi katika kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia", alisema Dkt. Shekalaghe.
Aidha, katika ziara hiyo Dkt. Shekalaghe alipata fursa ya kutembelea miundombinu ya LST ikiwemo jengo la mahakama ya kufundishia pamoja na kuwasalimia wanafunzi ambao aliwahimiza kusoma kwa bidii na kuzingatia maadili.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya LST, Prof. Sist Mramba alieleza kuwa Taasisi yake inajivunia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake na kubainisha mikakati ya muda mfupi na mrefu iliyowekwa na Taasisi katika kuendelea kuboresha utoaji mafunzo ya uanasheria kwa vitendo.
"Kwa kuwa Watanzania wanaohitaji huduma za kisheria na wanaotumia mawakili ni watu wanaoweka dhamana ya mali zao na maisha yao, imebidi taasisi yetu tuhakikishe tunazingatia ubora na vigezo ili wanaohitimu na kupewa leseni za uwakili au kufanya kazi za uhakimu waweze kutoa huduma bora kwa umahiri na weledi", alibainisha Prof. Mramba.


.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment