Farida Mangube, Morogoro
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Sokoine Memorial, katika eneo la Wami Sokoine, wilayani Mvomero, huku likiendelea na msako wa kubaini mahali alipopelekwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Andrew Kantimbo, Tukio hilo limetokea Oktoba 26, 2026, majira ya saa 9:00 alasiri, wakati mwanafunzi huyo akitoka shuleni na wenzake katika eneo la Wami Sokoine, Kata ya Dakawa.
Imedaiwa mwanafunzi huyo alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa kwa kutumia pikipiki kabla ya watu waliokuwa naye kutokomea kusikojulikana.
Wanaoshikiliwa na Polisi ni Kandolo Rosingo Kibasisi (56), mkazi wa Sokoine Shule, Michael Jackson Shabala (32), mkazi wa Victoria Ngale, pamoja na Hagiro (41), ambao wote wanatajwa kuwa wafugaji na wakazi wa Sokoine Shule.
Kamanda huyo wa Polisi amesema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini alipo mwanafunzi huyo na kuhakikisha wote waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Katika taarifa hiyo, Polisi wameeleza kuwa tukio hilo linahusishwa na mila potofu zinazodaiwa kuwepo katika baadhi ya maeneo ya jamii ya Kimasai, zinazohusisha kumchukua binti kwa nguvu anapokataa kuolewa kwa hiari, kisha familia kukutana na kujadiliana kuhusu mahari.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Kantimbo amewataka wananchi kuachana na mila zinazohatarisha usalama na haki za watoto, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kusimamia malezi na elimu ya watoto wao.
Aidha akawasihi wananchi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto, hususan wanafunzi wa kike, wanalindwa na kupewa mazingira salama ya kuendelea na masomo ili waweze kutimiza malengo yao na kuchangia maendeleo ya Taifa.


No comments:
Post a Comment