Na Saidina Msangi, WF, Arusha
Serikali imesema itaendelea kuboresha mfumo wa kodi nchini ili uwe wa haki na unaotabirika, unaochochea ukuaji wa biashara na uwekezaji, kwa lengo la kufikia azma ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kampuni ya Ernst & Young (EY) Tanzania, unaohusika na huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa hesabu na ushauri wa biashara. Mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya Gran Meliá jijini Arusha.
Munde alisema kufikiwa kwa malengo ya Dira 2050 kunahitaji juhudi za Serikali pamoja na ushirikiano wa karibu na sekta binafsi, ikiwemo kampuni zinazotoa huduma za kitaalamu.
Alisema ili kufikia uchumi wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, nchi inahitaji uwekezaji wenye tija kutoka sekta binafsi, taasisi imara na mfumo wa kodi unaochochea ushindani na ukuaji wa biashara.
Aliongeza kuwa Serikali imeazimia kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha walipakodi kutimiza wajibu wao kwa hiari.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akipokelewa na Mkuu wa Huduma za Kodi wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu, na ushauri wa kibiashara ya Ernst &Young-Tanzania, Bw. Donald Nsanyiwa, wakati alipowasili kwa ajili ya kufungua mkutano wa mwaka wa kampuni hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha.)
Munde alifafanua kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mapitio ya Mfumo wa Kodi, yakiwemo kuunganisha mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA), pamoja na kutenga asilimia tano ya rasilimali za serikali za mitaa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya masoko.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA na uchanganuzi wa takwimu ili kupunguza ulazima wa walipakodi kukutana ana kwa ana na maofisa wa kodi. Hatua nyingine ni kufanya ukaguzi wa pamoja baina ya taasisi za udhibiti.
Mkuu wa Huduma za Kodi wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu, na ushauri wa kibiashara ya Ernst &Young-Tanzania, Bw. Donald Nsanyiwa, akizungumza katika mkutano wa mwaka wa kampuni hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha.
Alisema Serikali pia itaendelea kutoa unafuu wa kodi wa mwaka mmoja kwa biashara ndogo zilizoanzishwa hivi karibuni ili kuzipa nafasi ya kukuza mitaji yao. Vilevile, itaendelea kutekeleza Mkakati wa MKUMBI II unaolenga kupunguza mlundikano wa ada na tozo, huku Wizara ya Fedha ikiwa imetenga sehemu maalumu ya mapato yasiyo ya kodi kwa ajili ya kuratibu eneo hilo.
Munde alizitaka taasisi za kitaalamu na washauri wa kodi kuendelea kutoa ushauri unaozingatia maadili, unaolinda uendelevu wa biashara na maslahi ya taifa. Pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa jamii.
Mshauri wa Huduma za Kodi wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu, na ushauri wa kibiashara ya Ernst &Young-Tanzania, Bi. Beatrice Melkiory, akizungumza katika mkutano wa mwaka wa kampuni hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha.
Aliwahimiza washiriki wa mkutano huo kutumia fursa hiyo kujadili sera za kodi, fursa za uwekezaji na namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa manufaa ya uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Kodi wa EY Tanzania, Donald Nsanyiwa, alisema mkutano huo unalenga kujenga mfumo wa kodi wenye ufanisi na uwazi unaochochea ukuaji wa uchumi wa taifa, huku ukiboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani bila kuathiri shughuli za sekta binafsi.
Nsanyiwa alisema majadiliano yatajikita katika maeneo matatu makuu, ambayo ni kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari, kuziandaa biashara kukabiliana na mabadiliko ya kisheria na kisera, pamoja na kujenga uaminifu kati ya walipakodi na TRA.
Alisema washiriki watajadili mbinu bora za kibiashara zinazoweza kuongeza utii wa sheria za kodi na wakati huohuo kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.
Aidha, watarejea hoja na mapendekezo ya kikodi yaliyojadiliwa mwaka uliopita, hatua zilizochukuliwa na Serikali na namna mabadiliko hayo yanavyoweza kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Nsanyiwa alisisitiza umuhimu wa majadiliano yenye kujenga ushirikiano kati ya wafanyabiashara, wataalamu wa kodi na Serikali, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji.
Alisema wataalamu wa kampuni hiyo watashirikisha uzoefu na maarifa kuhusu changamoto zinazojitokeza katika usimamizi na ulipaji kodi, pamoja na njia bora za kuzitatua ili wafanyabiashara waelewe mabadiliko yanayoendelea na kuwa tayari kuyatekeleza.
Pia alisema washiriki watapata fursa ya kuongeza uelewa kuhusu mifumo mipya ya kidijitali inayotumika katika usimamizi wa kodi, ili waweze kuitumia kwa usahihi na ufanisi.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Bolder Thinking, Smarter Tax, Stronger Future” uliwakutanisha washiriki kutoka sekta ya umma na binafsi, wanadiplomasia, wawekezaji na wataalamu wa kodi.
#TATS2026
#BolderSmarterStronger











No comments:
Post a Comment