HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 27, 2026

ELIMU YA UHASIBU YAWAFIKIA BAGAMOYO


 

Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kuimarisha juhudi za kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari na Taasisi za elimu ya juu nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza Taaluma ya Uhasibu na kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Bodi hiyo na fursa zilizopo katika Taaluma hiyo.

Katika mwendelezo wa juhudi hizo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bagamoyo wametembelea NBAA na kupatiwa mafunzo maalumu yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu shughuli za Bodi, majukumu yake na fursa mbalimbali za kitaaluma katika sekta ya Uhasibu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi, aliipongeza shule hiyo kwa kuwawezesha wanafunzi kupata elimu ya vitendo nje ya darasa, hususan wale wanaosoma masomo ya biashara na uhasibu. Aliwahimiza wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea, akisisitiza umuhimu wa Taaluma ya Uhasibu katika Taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

"Na pia kuanzia mwaka huu 2026 Bodi hii imeanzisha Tuzo maalumu kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, hususan katika masomo ya Uhasibu, ikiwa ni njia ya kutambua, kuhamasisha na kuendeleza Taaluma ya Uhasibu." alisema CPA Prof. Siasa I. Mzenzi

CPA Malendeja alieleza kuwa, kuwajengea wanafunzi msingi wa uhasibu katika hatua za awali za masomo kutawasaidia kujiandaa kuwa wataalamu bora wa baadaye ambapo alisisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili ya Taaluma hiyo, ikiwemo uadilifu, uaminifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii, akibainisha kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kulinda na kuendeleza hadhi ya Taaluma ya Uhasibu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya, alisema ziara hiyo imewapa wanafunzi fursa ya kupata taarifa sahihi kuhusu majukumu ya Bodi na kuelewa zaidi fursa zilizopo katika Taaluma ya Uhasibu. Aliongeza kuwa ziara za aina hiyo huwasaidia wanafunzi kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wao wa kitaaluma kwa kuhusisha maarifa wanayopata darasani na mazingira halisi ya kazi.

"Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za NBAA za kukuza Taaluma ya Uhasibu nchini kwa kuwajengea wanafunzi uelewa wa mapema kuhusu Taaluma hii na kuwaandaa wataalamu wenye maarifa, ujuzi na maadili yanayohitajika katika soko la ajira la ndani na nje yaani kitaifa na kimataifa, pamoja na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi." Alisema Magreth Kageya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA zilizopo jijini Dar es Salaam.
CPA Kulwa Malendeja, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara kutoka Shule ya Sekondari ya Bagamoyo waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za NBAA zilizopo jijini Dar es Salaam.
Magreth Kageya, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa NBAA akitoa mada kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na NBAA "NBAA Overview" kwa wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
Mfanyakazi wa NBAA, Humphrey Symphorian akitoa mada kuhusu njia za Taaluma katika uhasibu pamoja na mitihani ya kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
Mfanyakazi wa NBAA, CPA Amiri Mjema akitoa mada kuhusu Mirabaha ya uhasibu na uhasibu wa mishahara, pamoja na ukokotoaji wa kodi ya PAYE kwa wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo.
CPA. Bertha Kipangula, Mkuu wa Sehemu ya Usajili wa Wanachama, Uzingatiaji wa Sheria na Maendeleo ya Kitaaluma akitoa elimu kuhusu fursa za kazi katika mazingira halisi na muhtasari wa Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma (CPD) kwa wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo.
CPA Mike akitoa elimu kuhusu viwango vya Uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha kwa wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
Baadhi ya wafanyakazi wa NBAA na wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo wakifuatilia mada kwa wataalam kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) walipotembelea ofisi za Bodi hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa I. Mzenzi (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na CPA Kulwa Malendeja, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA (wa pili kulia waliokaa), walimu pamoja na wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari ya Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad