*Awatakaka kuongeza ubunifu
Na Mwandishi Wetu
WAJASIRIAMALI nchini, hususan wanawake, wametakiwa kuongeza juhudi na ubunifu katika shughuli zao za kiuchumi badala ya kukata tamaa na kulalamika wanapokutana na changamoto za kibiashara.
Wito huo umetolewa na mfanyabiashara Olivia Chagula wakati akizungumza na kundi la wajasiriamali wanawake katika eneo la Madale, Dar es Salaam, kwa lengo la kuwatia moyo na kuwahamasisha kuendelea kujituma ili kuongeza kipato.
Chagula, ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Ubunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2025, alisema amedhamiria kuwafikia wanawake wengi katika maeneo mbalimbali ili kuwahamasisha kujitegemea kiuchumi kupitia shughuli za ujasiriamali.
“Maono yangu ni kuwafikia akina mama wengi katika maeneo yetu, wilaya yetu na wilaya nyingine ili kuwapa moyo wa kuendelea kupambana katika shughuli zao za kiuchumi,” alisema Chagula.
Aliongeza kuwa juhudi za wanawake katika kufanya kazi na kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema ataendelea kutumia shughuli zake za kibiashara kuwahamasisha wanawake wajasiriamali kuongeza juhudi, kutafuta fursa mpya na kuimarisha biashara zao ili waweze kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.
Katika hatua nyingine, Chagula aliipongeza Serikali kwa kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa za El Niño, akiwataka wananchi kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za tahadhari kwa wakati.


No comments:
Post a Comment