HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 15, 2026

Benki ya Absa Yazindua Kampeni ya “Mkwanja Kilaini na Kadi ya Absa” kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali.

Benki ya Absa Tanzania imezindua kampeni iliyopewa jina la “Mkwanja Kilaini na Kadi ya Absa”, ikiwa na na lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali huku ikitenga jumla ya Shilingi milioni 60 kama zawadi za fedha taslimu kwa wateja wanaotumia kadi zake za malipo na mikopo katika miamala yao ya kila siku.

Kupitia kampeni hiyo itakayodumu kwa muda wa miezi mitatu itashuhudia washindi watatu wa kila mwezi wakijishinda pesa taslimu ambapo mshindi wa kwanza Shilingi milioni 5, mshindi wa pili Shilingi milioni 3 na mshindi wa tatu Shilingi milioni 2.

Jumla ya washindi tisa watapatikana katika kampeni hiyo ambapo zawadi kuu ya Shilingi milioni 30 itatolewa kwa mshindi mmoja mwishoni mwa kampeni, na kufanya jumla ya zawadi zote kufikia Shilingi milioni 60.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wateja Binafsi, Mkuu Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Heristraton Genesis, alisema kampeni hiyo inaakisi dhamira ya benki ya kuwazawadia wateja wake huku ikihamasisha matumizi ya huduma za kibenki zilizo salama na rahisi zaidi.

“Katika Absa, tunaendelea kutafuta njia bunifu za kuwazawadia wateja wetu huku tukihamasisha tabia bora za kifedha. Kupitia kampeni ya ‘Mkwanja Kilaini, na Kadi ya Absa’, wateja wanachotakiwa kufanya ni kutumia kadi zao za Absa za malipo au mikopo katika manunuzi na miamala yao ya kila siku ili kupata nafasi ya kushinda zawadi za fedha taslimu zinazoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yao,” alisema.

Genesis aliongeza kuwa kadiri wateja wanavyofanya miamala mingi zaidi inayokidhi vigezo vya kampeni hiyo, ndivyo wanavyoongeza nafasi zao za kushiriki katika droo za bahati nasibu na kushinda zawadi.

Alibainisha kuwa malipo kwa kutumia kadi yana faida mbalimbali, zikiwemo urahisi wa matumizi, usalama ulioimarishwa, kukubalika katika maeneo mbalimbali duniani na kurahisisha upatikanaji wa huduma za biashara za kidijitali. Alisema faida hizo zinaifanya njia hiyo kuwa chaguo linalofaa zaidi katika uchumi wa kisasa unaozidi kutegemea teknolojia.

Kampeni hiyo inawahusu wateja waliopo na wapya wa Absa wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao wanamiliki kadi za benki za malipo au mikopo za Absa. Wateja wanapaswa kufanya miamala inayokidhi vigezo vya kampeni kwa kutumia kadi zao na njia za huduma za kibenki za kidijitali zinazostahili ndani ya kipindi cha kampeni.

Washindi watapatikana kupitia droo za bahati nasibu zitakazofanyika kila mwezi chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Abigail Lukuvi, alisema kampeni hiyo inasisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuwaweka wateja katika kiini cha shughuli zake zote.

Alisema mpango huo unafuatia Wiki ya Huduma kwa Wateja, lakini unaonyesha kuwa juhudi za benki hiyo za kutambua na kuthamini wateja wake zinaendelea hata baada ya maadhimisho hayo ya kila mwaka.

“Wateja wetu ndio kiini cha biashara yetu, na kampeni ya ‘Mkwanja Kilaini, na Kadi ya Absa’ ni fursa nyingine kwetu ya kuwatambua, kuwazawadia na kuthamini imani wanayoendelea kutupatia kila siku,” alisema Abigail.

Aliongeza kuwa Absa imekuwa ikiendesha kampeni za kuwazawadia wateja kwa miaka mitatu mfululizo, huku kampeni zilizotangulia zikiwa na zawadi kubwa za fedha taslimu pamoja na zawadi nyingine zenye thamani, zikiwemo magari.

Kwa mujibu wa Abigail, kampeni hizo zinaunga mkono dhamira ya benki hiyo ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho pamoja… Hatua moja baada ya nyingine”, kwa kutambua wateja wake na kuwasaidia kufikia malengo yenye umuhimu katika maisha yao.

Kampeni hiyo mpya pia ni sehemu ya mkakati mpana wa Absa wa kuongeza matumizi ya huduma za kibenki za kidijitali na kuhamasisha malipo yasiyotumia fedha taslimu katika matumizi ya kila siku, manunuzi ya mtandaoni na miamala ya biashara.
01: Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (kushoto), akizungumza jijini Dar es Saaam leo, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itakayodumu kwa muda wa miezi mitatu. Kulia ni Meneja Bidhaa za Kadi, Bi. Erica Mwaipopo.

Meneja Bidhaa za Kadi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Erica Mwaipopo (kulia), akizungumza jijini Dar es Salaam leo, katika uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itkayodumu kwa muda wa miezi mitatu. Kulia kwake ni Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi, Bw. Heristraton Genesis na wafanyakazi wengine wa benki hiyo.

Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (wa nne kutoka kushoto, waliokaa), pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Absa, wakipozi mbele ya wapigapicha, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itkayodumu kwa muda wa miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad