Absa Bank Tanzania imeahidi kuimarisha huduma kwa wateja kwa kusikiliza kwa karibu zaidi maoni yao na kuyatumia kuboresha ubora na mwitikio wa huduma zake.
Ahadi hiyo ilitolewa leo wakati benki hiyo ilipozindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, iliyobeba kaulimbiu ya “Extra Mile”, ikisisitiza umuhimu wa kwenda hatua ya ziada katika kuwahudumia wateja.Akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Bank Tanzania, Obedi Laiser, alisema benki hiyo inatambua kuwa wateja wanatarajia zaidi ya bidhaa za kifedha, huku uzoefu wa huduma ukiendelea kuwa sehemu muhimu ya uhusiano wao na taasisi za fedha.
“Kila mteja ana hadithi yake, na kila mwingiliano tunaokuwa nao na mteja huyo unakuwa sehemu ya hadithi hiyo. Absa, ahadi ya chapa yetu ni rahisi: "Story yako ina Thamani” alisema.
Laiser alisema wateja huja katika benki wakiwa na malengo, changamoto na matarajio tofauti ya kifedha, hivyo wafanyakazi wanapaswa kusikiliza kwa makini, kuitikia kwa wakati na kuwajibika katika kushughulikia masuala yanayowasilishwa na wateja.
Alisema kwenda hatua ya ziada si lazima kuhusishe mambo makubwa, bali ni kuhakikisha huduma inayotolewa kwa wateja inakuwa ya haraka, inayozingatia mahitaji binafsi na yenye ufanisi.
“Utamaduni wa taasisi hatimaye unaonekana kupitia uzoefu wa mteja. Unaonekana katika namna tunavyojibu kwa haraka, tunavyoshirikiana kwa ufanisi, iwapo tunachukua jukumu pale changamoto zinapotokea, na kama tuko tayari kwenda zaidi ya kiwango cha chini kinachohitajika ili kupata suluhisho,” alisema.
Laiser alisema kila mfanyakazi ana nafasi katika kujenga uzoefu mzuri wa mteja, bila kujali kama anahudumia wateja moja kwa moja au anafanya kazi nyuma ya pazia.
Alisema benki hiyo pia inatambua umuhimu wa kuweka uwiano kati ya ubunifu wa kiteknolojia na mwingiliano wa kibinadamu, huku matarajio ya wateja yakiendelea kubadilika.
“Wajibu wetu ni kuunganisha teknolojia na uhusiano wa kibinadamu, ufanisi na uelewa wa mahitaji ya mteja, pamoja na ubunifu na uaminifu,” alisema.
Katika hatua nyingine benki hiyo pia iliwatambua wafanyakazi kutoka vitengo mbalimbali kwa mchango wao katika huduma kwa wateja, wakiwemo wale ambao kazi zao hazionekani moja kwa moja na wateja, lakini ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Laiser alisema benki hiyo inathamini imani ambayo wateja wameiweka kwake kwa kukabidhi biashara zao, familia zao na matarajio yao ya kifedha kwa Absa.
Alisema kaulimbiu ya “Extra Mile” haipaswi kuishia katika maadhimisho ya wiki hiyo pekee, bali inapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa kila siku wa benki katika kuwahudumia wateja.
Mteja wa muda mrefu wa benki hiyo, Hilary Biduga, mfanyabiashara katika sekta za utalii na usafirishaji, aliipongeza benki hiyo kwa kile alichokiita huduma za haraka na zenye ufanisi, hususan katika mazingira yanayohitaji hatua za haraka.
Hata hivyo, Biduga alieleza wasiwasi kuhusu upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wateja wenye umri mkubwa, hususan wastaafu na wamiliki wa biashara.
Aliitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ina jukumu la kusimamia sera ya fedha, pamoja na mamlaka nyingine husika, kulichunguza suala la ukomo wa umri katika utoaji wa mikopo.
“Wateja wengi wenye umri mkubwa, wakiwemo wastaafu, wanamiliki biashara kubwa na wana ukwasi mkubwa. Kwa hiyo, kwa nini unapoenda benki wanafurahi kupokea fedha zako, lakini unapokwenda kuomba mkopo wanaambiwa kuwa tayari umefikia umri wa miaka 65 na hivyo unawekwa katika kundi la wateja wenye hatari kubwa?” alisema.
Alieleza kuwa uwezo wa kifedha na uwezo wa mteja mmoja mmoja kurejesha mkopo pia vinapaswa kuzingatiwa wakati wa kutathmini maombi ya mikopo.
Awali, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Ndabu Lilian Swere, alisema maoni ya wateja yaliyokusanywa wakati wa wiki hiyo yatatumika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
“Tutatumia maoni kutoka kwa wateja wetu kuhakikisha tunaendelea kuboresha huduma zetu na kutoa uzoefu bora zaidi kwa wateja,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser ( kulia) akikabidhi cheti kwa mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo, Bi. Suma Poland kwa kutambua utendaji kazi wake bora katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja, katika Tawi la Mikocheni, jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Swere.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser ( wa pili kulia) akigawa chakula kwa baadhi ya wateja waliohudhuria uzinduzi Wiki ya Huduma kwa Wateja ya benki hiyo, katika Tawi la Mikocheni, jijini Dar es Salaam leo.

No comments:
Post a Comment