HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 7, 2026

TMDA, Polisi Waanzisha Mkakati wa Kudhibiti Dawa Bandia Nchini

Na Emmanuel Massaka, Michuzi TV

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kudhibiti uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa za tumbaku zisizokidhi viwango nchini.

Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo, amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanatumia bidhaa zilizo na ubora, usalama na ufanisi unaokubalika.

Akizungumza katika kikao kazi kati ya TMDA na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, Fimbo alisema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango haziingii wala kuendelea kuwepo katika soko.

“Majukumu yetu makubwa ni kuhakikisha bidhaa hizo ni bora, salama na zina ufanisi kwa matumizi ya binadamu na mifugo,” alisema.

Alisema kabla ya bidhaa kuingia nchini, zinapaswa kusajiliwa na TMDA na kufanyiwa tathmini kupitia tafiti na uchunguzi wa kitaalamu ili kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi wake.

Aidha, alisema TMDA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya jumla na rejareja pamoja na maeneo mengine ya usambazaji, kuhakikisha bidhaa zinazouzwa ni zile zilizosajiliwa na kuruhusiwa kuingia sokoni.

Fimbo alisema TMDA pia huchukua sampuli za bidhaa kutoka maeneo mbalimbali na kuzipeleka katika maabara zake kwa uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini kama zinakidhi viwango vilivyowekwa.

Alisema sampuli zinazokamatwa na Jeshi la Polisi wakati wa operesheni na doria mbalimbali pia huwasilishwa TMDA kwa ajili ya uchunguzi, hatua inayowezesha mamlaka kutoa ushahidi wa kitaalamu unaoweza kutumika katika kesi mahakamani.

“Jeshi la Polisi linapokamata sampuli mbalimbali, huletwa kwetu kwa ajili ya kuthibitisha kama zinakidhi viwango vya ubora. Uchunguzi huu hutuwezesha kutoa vielelezo vinavyoweza kutumika kwenye kesi mbalimbali mahakamani,” alisema.

Bidhaa zisizokidhi viwango kuondolewa sokoni

Fimbo alisema TMDA ina jukumu la kuondoa sokoni bidhaa zisizokidhi viwango na kuziteketeza katika maeneo maalumu ili kuzuia zisirejee tena sokoni na kuhatarisha afya za wananchi.

Alisema mamlaka hiyo pia hushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi nyingine za Serikali katika vituo vya mipakani, kwa lengo la kudhibiti uingizaji wa bidhaa hizo nchini.

Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi na askari wa Jeshi la Polisi kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wakiwamo makamanda wa Polisi wa mikoa ya Temeke, Kinondoni na Ilala pamoja na wakuu wa upelelezi wa mikoa hiyo.

Fimbo alisema kikao hicho ni sehemu ya mpango wa TMDA wa kuimarisha uhusiano na Jeshi la Polisi, ambapo mamlaka hiyo imeanza kufanya vikao vya aina hiyo katika kanda zake na inatarajia kuviendesha pia katika mikoa mingine nchini.

“Tumekuwa tukifanya vikao kazi na waandishi wa habari katika kanda mbalimbali Tanzania, lakini hatujawahi kufanya vikao kama hivi na Polisi. Tumeona umuhimu wa kuanza utaratibu huu ili tukutane, tujenge uelewa na kujadili kwa pamoja namna ya kudhibiti bidhaa hizi,” alisema.

Alisema TMDA ina kanda nane nchini na inatarajia kufanya vikao hivyo kila mwaka ili kuongeza uelewa wa majukumu ya kila upande na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa sheria.

Mbali na udhibiti wa bidhaa hizo, Fimbo alisema TMDA pia inasimamia majaribio ya dawa yanayofanyika kwa wanyama, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya dawa na bidhaa nyingine zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.







 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad