
Na Mwandishi Wetu, Algiers
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, amesema hayo Septemba 30, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Algeria katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers.
Amesema hatua hizo zimefikiwa katika kipindi cha miezi michache iliyopita kufuatia maelekezo ya viongozi wa nchi hizo mawili ya kuhakikisha maeneo yaliyobainishwa ya ushirikiano yanaanza kutekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya wananchi.
“Nilipowasilisha hati zangu za utambulisho mnamo tarehe 10 Juni, 2026, Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kwamba sasa umefika wakati wa kuuweka ushirikiano wetu katika vitendo na wakati nikija Algeria Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kwamba kutokana na ushirikiano wetu wa kimkakati sasa ni wakati wa kupata manufaa kwa ajili ya wananchi wetu,” amesema.
Katika sekta ya viwanda vya dawa, Balozi Matinyi amesema Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) pamoja na Saidal Group vinatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Oktoba kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), kwa ajili ya kujadili maeneo ya ushirikiano wa kitaalamu.
Amesema kampuni ya Hikma pia ipo katika hatua za mwisho kukamilisha makubaliano ya ushirikiano katika biashara na uwekezaji na Medipharm, kampuni tanzu ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), huku kampuni ya Frater Razes ikitarajiwa kuja Tanzania mwezi Oktoba kwa ajili ya majadiliano ya ushirikiano wa biashara na uwekezaji.
Kwa upande wa nishati, Balozi Matinyi amesema Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), kampuni tanzu ya TANESCO, ilifanya ziara nchini Algeria mwezi Julai 2026 kwa ajili ya kujadili ushirikiano wa kitaalamu na kutembelea maeneo ya kiufundi ya SONELGAZ pamoja na kiwanda cha vifaa vya umeme cha GISB Electric.
Katika sekta ya elimu ya juu, amesema Algeria imetoa nafasi 176 za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, ambapo Serikali imechagua wanafunzi 150 wenye ufaulu wa juu chini ya mpango wa Samia Scholarship Extended.
Amesema wanafunzi hao watasoma katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba.
Kuhusu biashara ya mazao ya kilimo, Balozi Matinyi amesema kampuni ya Sarl Anacard’Or ya Algeria imenunua ghala la kuhifadhia korosho mkoani Mtwara kwa ajili ya kusafirisha korosho hizo kwenda Algeria, huku ikiendelea na mipango ya kuanza ubanguaji wa korosho nchini Tanzania.
Aidha, amesema kampuni ya CAM Sarl ya Algeria, inayotengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo na dawa pamoja na vifaa vya kufungashia, imekubali kushirikiana na Tanzania katika upatikanaji wa mashine hizo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa katika soko la dunia.
Katika sekta ya ufugaji wa nyuki, Balozi Matinyi amesema Tanzania na Algeria zinatarajia kuanza ushirikiano baada ya maafisa na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TFS pamoja na wadau wa sekta binafsi kufanya ziara nchini Algeria mwezi Septemba 2026.
Amesema wakati wa ziara hiyo, wataalamu wa nchi hizo walikubaliana kuanza ushirikiano katika ufugaji wa nyuki na mazao yake.
Balozi Matinyi pia amewakaribisha wananchi wa Algeria kutembelea Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, eneo la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro pamoja na fukwe za Zanzibar.

No comments:
Post a Comment