VIJANA 50 wenye ufaulu wa juu lakini wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kifedha watanufaika na uwezeshaji wa elimu ya chuo kikuu na maandalizi ya kuingia katika soko la ajira.
NMB Foundation (NMBF), ikishirikiana na Benki ya NMB, imetenga Sh bilioni 1 kuwawezesha vijana hao kupitia dirisha la tatu la programu ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship kwa mwaka wa masomo 2026/27.Maombi yote yatapokelewa kupitia tovuti ya NMB Foundation, foundation.nmbbank.co.tz, kuanzia leo hadi tarehe 18 Septemba 2026.
Programu hiyo inalenga Watanzania waliomaliza Kidato cha Sita mwaka huu kwa Daraja la Kwanza lenye pointi tatu hadi tano. Waombaji pia wanapaswa kuwa na ushahidi wa uhitaji wa kifedha na kutarajia kujiunga na taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alisema vijana watakaochaguliwa wataungana na wanufaika 101 waliowezeshwa kupitia awamu mbili zilizopita.
Kwa kuongezwa vijana hao 50, idadi ya wanufaika wa programu hiyo itafikia 151. NMBF imetumia zaidi ya Sh bilioni 2.1 katika awamu zilizopita, huku Sh bilioni 1 zikitengwa kwa kundi jipya.
“Uwezeshaji huu utagharamia ada, fedha za kujikimu, mafunzo kwa vitendo, malipo ya lazima ya chuo na vifaa vya kujifunzia, ikiwemo kompyuta mpakato,” alisema Karumuna.
Alisema vijana watakaopatikana pia watapatiwa malezi na ushauri wa kitaaluma, mafunzo ya uongozi, maandalizi ya kuingia katika soko la ajira na fursa za kujifunza kwa vitendo.
Karumuna alisisitiza kuwa maombi hayana gharama na hakuna mtu wala taasisi iliyopewa mamlaka ya kuuza nafasi hizo. Uchaguzi utafanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na uhakiki wa kina ili kuhakikisha fursa zinawafikia walengwa.
Programu ya Nuru Yangu ilianzishwa Mei 19, 2022, ikiwa na lengo la kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowazuia vijana wenye uwezo mkubwa kitaaluma kuendelea na elimu ya juu.
Mmoja wa wanufaika wake, Elia Johnson Kaberege, aliyehitimu Shahada ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2025, alisema programu hiyo ilimwezesha kumudu gharama za masomo na mahitaji mengine ambayo familia yake isingeweza kugharamia.
Naye Irene John Busorwa, mhitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema alikaribia kukosa nafasi ya kujiunga na chuo kutokana na hali ya kifedha ya familia yake. Kupitia Nuru Yangu, aliweza kusoma kwa miaka mitatu na kuhitimu. Kwa sasa ameajiriwa katika kampuni ya ukaguzi wa hesabu.
NMBF, ikishirikiana na Benki ya NMB, imewataka vijana wenye sifa kutuma maombi kupitia tovuti rasmi pekee kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo Septemba 18, 2026.

.jpeg)


.jpeg)

No comments:
Post a Comment