Na mwandishi wetu
Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi akimkabidhi tuzo Msemaji wa Kampuni ya Alliance One Wakili John Magoti(kulia), ambaye kampuni yake imetwaa nafasi ya Mshindi wa Pili wa Jumla wa Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa mwaka pamoja na mshindi wa Kwanza wa Sekta ya Uchakataji Tumbaku, huku Waziri wa Viwanda na Biashara Wakili Judith Kapinga akishuhudia.
Makamu wa Rais Degratius Ndejembi amewaasa wazalishaji wa viwanda nchini kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa nchini, unalenga kuwapunguzia mzigo wa gharama za maisha watanzania.
Amesema hayo kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji bora za mwaka huu, ambapo Makamu wa Rais amemwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.Katika tuzo hizo kampuni ya tumbaku ya Alliance One, imekuwa kinara wa tuzo hizo kwa kushika nafasi ya mshindi wa pili wa jumla ya tuzo zote, lakini pia imeshinda tuzo ya mzalishaji bora wa uchakatataji tumbaku.
Akitoa mfano amesema wazalishaji wa simenti nchini wanapaswa kuongeza ushirikiano kata yao na wauza malighafi, ikiwemo klinka na malighafi nyingine, lengo likiwa kushusha gharama bidhaa hiyo, sambamba na maelekezo ya Rais kwamba wananchi waipate bidhaa hiyo kwa bei ya awali ambayo ilikuwa ni ndogo.
“Katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania, sekta ya viwanda ina nafasi kubwa sana,na duniani kote sekta ya viwanda ndiyo chimbuko la mandeleo ya haraka mhimiri mkuu wa uongezaji thamani wa malighafi zilizopo nchini na mtoaji wa ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya serikali pampja na fedha za kigeni,”amesema.
Ameipongeza kauli mbiu tuzo hizo mwaka huu ambayo ni kuhamasisha uendelevu,uwajibikaji na ustahimilivu katika uzalishaji viwandani, kwani inanenda sambamba na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 ikichagiza na kuchochea mageuzi endelevu ya viwanda hapa nchini.
“Kutokana na wingi wa raslimali tulizonazo hapa nchini ikiwemo misitu na madini mbalimbali ni muhimu kukuza sekta ya viwandana kuendelea kujenga mahusiano na sekta ya viwanda na sekta nyingine ili kuongeza ufanisi na kuharakisha maendeleo jumuishi na hatimaye kuongeza kipato cha watanzania walio wengi,”amesema.
Amesema serikali za inatambua na kuunga mkono juhudi za sekta ya uzalishaji nchini, kwani kutokana na hilo, mchango wa sekta uzalishaji viwandani kwenye pato la taifa mwaka 2025 ulifikia asilimia 5.9 na pia asilimia 12 mpaka 22 ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi kwenye mwaka huo zilikuwa za viwandani.
Hata hivyo aliwaasa wenye viwanda nchini kuongeza uzalishaji hatimaye waweze kupenya na kukabiliana na ushindani kwenye masoko ya nchi jirani na siyo kuzalisha bidhaa za soko la hapa nchini peke yake.
Akiongea baada ya kupokea tuzo hiyo, Msemaji wa Alliance One Wakili John Magoti ameishukuru serikali ya awamu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi na biashara nchini yanayowezesha uwekezaji katika uzalishaji bora na endelevu.
“Sisi Alliance One tumeipokea tuzo hii kwa bashasha sana tukiamini kwamba imepatikana kutokana na uwajibikaji wa pamoja kati yetu sisi wafanyakazi wa kudumu wapatao 350 pamoja na wale msimu 4,600 na wadau wengine ambao ni wakulima wa tumbaku zaidi ya laki moja, na kiukweli tuzo hii ni yetu sote kwa pamoja,” amesema.
Amesema kampuni hiyo imeboresha uzalishaji ikiwemo matumizi ya umeme jua kiwandani nyakati za mchana na pamoja na matumizi ya gesi asilia kwenye magari na baadhi ya mitambo kiwandani hapo.
“Tumefanya hivyo ili kwenda sambamba na mdundo wa dunia ambao ni utunzaji wa mazingira na upunguzaji wa gesi ya ukaa wakati huo huo tukiongeza tija na kuokoa baadhi ya gharama ambazo sasa tunazirejesha kwa wananchi kama misaada kwa jamii ambapo kila mwaka tunatenga zaidi ya milioni 500 kusaidia jamii kwenye elimu,maji na mazingira,” amesema.
Washindi wengine wa Tuzo za 19 za Mzalishaji bora ni Sili Africa ambaye ni mshindi wa Jumla huku Kiwanda cha Sigara kikishika nafasi ya Tatukwenye tuzo hizo zinazoratibiwa na Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI).
Akongea kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa CTI Sufian Ally ameiomba serikali kuongeza mapambano dhidi ya bidhaa bandia zinazoathiri soko la bidhaa za viwandani.
Aidha, ameiomba serikali kuendelea kuweka mazingira ya mazuri ya uzalishaji ikiwemo kupunguza gharama za uzalishaji kwa kutazama upya gharama za umeme,kumaliza tatizo la ucheleweshaji wa uondoaji bidhaa kutoka bandarini,pamoja na ushiriki wa kampuni za kitanzania kwenye tenda mbalimbali mambo ambayo Makamu wa Rais amesema serikali inaenda kuyafanyia kazi.



No comments:
Post a Comment