Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amelipongeza Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) kwa Tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora Viwandani (PMAYA), akisema zimekuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya viwanda tangu kuanzishwa kwake miaka 19 iliyopita.
Alitoa pongezi hizo Septemba 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo, ambapo Kampuni ya SILAFRICA Tanzania Limited iliibuka mshindi wa kwanza wa jumla, huku Alliance One ikiwa mshindi wa pili na Tanzania Cigarette PLC ikishika nafasi ya tatu.
Kampuni ya vinywaji ya Bonite Bottlers Limited iliibuka mshindi kwa upande wa kampuni kubwa zinazotengeneza vinywaji visivyo na kilevi.
Makamu wa Rais alisema sekta ya viwanda imeendelea kukua kwa kasi na viashiria mbalimbali vya uchumi vinaonyesha mafanikio chanya ya sekta hiyo, akitolea mfano mwaka 2025 ambapo sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 5.2, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.2 mwaka 2024.
Aidha, alisema mchango wa sekta ya uzalishaji katika Pato la Taifa mwaka 2025 ulifikia asilimia 5.9 na kwamba inakadiriwa kuwa asilimia 12 ya ajira rasmi na bidhaa zilizokuwa zinauzwa nje zilikuwa za viwandani.
“Haya ni mafanikio makubwa kwa takwimu, lakini lazima tujiulize viwanda vyetu vimekua kwa kiasi gani na je, ukuaji huu unaviwezesha kuwa na ushindani Afrika Mashariki na duniani na je, tunajipima kwa hayo au bado tunazalisha kwa kuangalia soko la ndani peke yake?” alihoji Makamu wa Rais.
Aidha, aliiitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa na wazalishaji wa saruji kuweka mipango ya kuhakikisha saruji inapatikana kwa wingi na inashuka bei na kurejea ilivyokuwa.
Alisema hivi sasa Watanzania wanalazimika kununua saruji kwa gharama kubwa kutokana na viongozi kushindwa kuratibu vyema uzalishaji wa bidhaa hiyo viwandani.
“Haya yanasababisha uhaba wa saruji na anayeumia hapa ni Mtanzania wa kawaida na Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo yake, anataka kuona Mtanzania anapata mfuko wa saruji kwa gharama nafuu,” alisema na kuongeza:
“Sasa nakuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, namwona hapa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kaeni pamoja mmalize hili suala ili Mtanzania apate saruji bei iliyokuwepo.”
“Nataka kuona maono ya Rais Samia kutaka Mtanzania wa kawaida anapata saruji kwa bei ya kawaida yanatekelezeka na ninataka kupata ripoti ya suala hilo baada ya kikao hiki. Kaeni mjadili suala hili na muandike ripoti tumkabidhi Rais,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga, alisema PMAYA inalenga kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Alisema tuzo hizo pia ni jukwaa la wazalishaji na wadau wa viwanda kukutana, kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuendeleza sekta hiyo.
Tenga alisisitiza kuwa tuzo hizo zinapaswa kuwa kichocheo cha kuongeza tija, ubunifu na ushindani katika uzalishaji wa viwandani.
Aidha, Tenga alisisitiza umuhimu wa uzalishaji endelevu unaozingatia mazingira, Environmental, Social and Governance (ESG), akisema ESG inazidi kuwa muhimu katika upatikanaji wa fedha, uwekezaji, masoko na kuingia katika minyororo ya thamani ya kimataifa.
Alisema kwa PMAYA 19, CTI imeanzisha Mabalozi 10 wa ESG, ambao watafuatiliwa kwa mwaka mmoja ili kupima utekelezaji na matokeo ya kanuni hizo katika kampuni zao.
Alisema kampuni itakayofanya vizuri zaidi itatambuliwa kama ESG Champion katika PMAYA 20.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment