HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 7, 2026

IFAD yataka uwekezaji zaidi katika kilimo na uvuvi Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Ujumbe kutoka International Fund for Agricultural Development (IFAD) pamoja na wataalamu kutoka sekta zinazotekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), wamekutana mkoani Tanga kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa programu hiyo na kutathmini mafanikio yaliyopatikana.

Timu hiyo pia inatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali yanayotekeleza AFDP mkoani Tanga, ikiwemo Kata ya Msomela katika Halmashauri ya Handeni Vijijini, ambako programu imehamasisha jamii ya Kimasai kushiriki katika kilimo bora.

Kupitia programu hiyo, jamii hiyo ambayo kwa asili ni wafugaji imeanza kujihusisha na kilimo cha mahindi chenye tija. Aidha, AFDP imewezesha kuanzishwa kwa mashamba darasa (FFS) kwa ajili ya mazao ya alizeti, mahindi na maharage.
Mashamba hayo yameonyesha mafanikio makubwa, ambapo hekta moja imekuwa na uwezo wa kuzalisha takribani magunia 20 ya mahindi, kila moja likiwa na uzito wa kilogramu 100. Hatua hiyo imewezesha jamii kupata chakula na kuongeza shughuli za kiuchumi kupitia kilimo.

Kwa upande wa sekta ya uvuvi, AFDP inaendelea na ujenzi wa Soko la Kimataifa la Samaki Kipumbwi katika Halmashauri ya Pangani. Ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 68 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.
Programu hiyo pia inaendelea na ujenzi wa vichanja 40 vya kukaushia dagaa, ambavyo kwa pamoja vina uwezo wa kukaushia takribani tani tano za dagaa kwa wakati mmoja.

Aidha, AFDP inaendelea na ujenzi wa ghala la baridi pamoja na mtambo wa barafu katika soko hilo, hatua inayolenga kuboresha uhifadhi na usafirishaji wa samaki na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Awali, Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini, Seth Meng, alikutana na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Emmanuel Kisongo, na kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa programu hiyo mkoani humo pamoja na mafanikio yanayotarajiwa kwa wananchi wa maeneo yanayonufaika.

Kaimu Katibu Tawala huyo alisema AFDP ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta za kilimo na uvuvi mkoani Tanga, huku akiishukuru IFAD kwa juhudi za kuwafikia wananchi na kuomba uwekezaji zaidi uongezwe mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad