Na Mwandishi Wetu
TEKNOLOJIA na matumizi jumuishi ya mtandao vinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuondoa vikwazo vinavyowakabili watu wenye mahitaji maalum katika elimu, ajira na kujiajiri, wadau wa Internet Governance wamesema.
Akizungumza katika mafunzo ya Tanzania School of Internet Governance, mtaalamu wa masuala ya Ujumuishwaji amesema Profesa Cosmas Mnyanyii watu wenye ulemavu, hususan wasioona na viziwi, bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata ajira katika sekta mbalimbali, hali inayohitaji matumizi zaidi ya teknolojia kuwawezesha kujitegemea.
Amesema tafiti na uzoefu unaonyesha kuwa watu wenye ulemavu mara nyingi hujikuta wakifanya kazi chache zisizohitaji ujuzi mkubwa, hivyo teknolojia inapaswa kutumika kuwapa ujuzi unaowawezesha kushindana katika soko la ajira na kujiajiri.
Kwa mujibu wake, mafunzo ya matumizi ya kompyuta kwa wasioona na viziwi yameonyesha kuwa teknolojia inaweza kuwawezesha kufanya kazi kwa kujitegemea bila kutegemea wasaidizi, akitoa mfano wa watu waliopata mafunzo na sasa wanaweza kwenda kazini na kutekeleza majukumu yao wenyewe.
Amesema Internet Governance ina uhusiano mkubwa na digital inclusion, kwa kuwa usimamizi mzuri wa mtandao unapaswa kuhakikisha makundi yote katika jamii, wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, yanapata fursa sawa za kutumia teknolojia na kunufaika na uchumi wa kidijitali.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuandaa mfumo maalum wa kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu, ikiwamo kuwafundisha viziwi kupitia viziwi wenzao na wasioona kupitia wasioona wenzao, hasa katika matumizi ya teknolojia na ujuzi wa kujiajiri.
Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kutatua changamoto zinazotokana na upungufu wa walimu wenye uwezo wa kutumia lugha na mbinu zinazofaa kuwafundisha watu wenye mahitaji maalum, huku ikiongeza idadi ya watu wenye ulemavu wanaoweza kuingia katika sekta za TEHAMA.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, College of ICT, Dkt.Joseph Mushi amesema chuo hicho kinashirikiana na Tanzania Internet Governance Chapter kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa, ikiwamo kupitia mafunzo na uboreshaji wa mitaala.
Amesema UDSM imekuwa ikifanya mapping kati ya mahitaji yanayotokana na sekta ya TEHAMA na yale yanayojadiliwa kupitia Internet Governance, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na fursa za kidijitali.
Naye Mkurugenzi wa Internet Society Tanzania Chapter, Dkt. Nazarius Kirama, amesema Tanzania School of Internet Governance inalenga kuwawezesha wananchi kutoka makundi mbalimbali kuelewa kuwa usimamizi wa Internet si jukumu la mtu mmoja, bali ni suala linalohitaji ushiriki wa Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, wataalamu, vyuo na wananchi.
Amesema elimu ya kidijitali inapaswa kupewa kipaumbele ili wananchi waweze kutumia Internet kama fursa ya elimu, ajira na ujasiriamali, huku akitoa wito kwa Serikali na wadau wengine kushirikiana kuhakikisha digital inclusion inafikiwa katika maeneo yote nchini.




No comments:
Post a Comment