SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika bandari kavu, maeneo ya kuhifadhi makontena na miundombinu ya maegesho ya malori ili kukabiliana na ongezeko la mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
TASAC imesema ongezeko la idadi ya makontena yanayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam linatokana na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji pamoja na maboresho yaliyofanyika katika huduma za bandari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema kuongezeka kwa shughuli za bandari kumeongeza mahitaji ya malori na maeneo ya kuhifadhi makontena.
Amesema maboresho hayo yameongeza ufanisi wa huduma za bandari, ikiwemo kupunguza muda wa
kuhudumia meli na upakuaji wa makontena.
Kwa mujibu wa TASAC, mwezi Julai pekee Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia takribani makontena 137,000, hali inayoonyesha kuongezeka kwa shughuli za biashara kupitia bandari hiyo.
TASAC imeeleza kuwa ongezeko hilo linahitaji maandalizi zaidi katika miundombinu ya usafirishaji na uhifadhi wa makontena, hususan kuongeza idadi ya malori na maeneo ya bandari kavu.
“Wenye bandari kavu wanapaswa kuongeza maeneo kwa ajili ya malori. Hii ni fursa na siyo laana,” imeelezwa.
Shirika hilo pia limewataka wamiliki wa bandari kavu kupanua maeneo ya maegesho ya malori na kuongeza uwezo wa kuhifadhi makontena ili kusaidia kupunguza msongamano katika maeneo ya bandari.
TASAC imesisitiza kuwa ongezeko la makontena ni fursa ya kiuchumi inayopaswa kuungwa mkono na sekta binafsi kupitia uwekezaji katika bandari kavu, malori na maeneo ya kuhifadhi makasha.
Aidha, TASAC imeonya dhidi ya taarifa na kauli zinazoweza kutoa taswira hasi kuhusu shughuli za Bandari ya Dar es Salaam, ikisema baadhi ya kauli zinaweza kupotosha mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za bandari.
Kwa upande mwingine, TASAC imeeleza kuwa kwa kushirikiana na waendeshaji wa bandari, ikiwemo DP World, uwezo wa kuhudumia meli umeongezeka, huku baadhi ya meli kubwa zikihudumiwa ndani ya muda mfupi.
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Abed Gallus, amesema mamlaka hiyo inaendelea kujiandaa kukabiliana na ongezeko la mizigo kwa kuboresha uwezo wa kuhifadhi na kuhamisha makontena kutoka eneo moja kwenda jingine ndani ya bandari.
TASAC imeeleza kuwa meli yenye takribani makontena 3,000 inaweza kuhudumiwa ndani ya siku moja, hatua inayosaidia kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shughuli za Bandari ya Dar es Salaam zimeendelea kukua, huku ongezeko la mizigo likiongeza mahitaji ya miundombinu ya usafirishaji na uhifadhi.
Katika upande wa bandari kavu, Bandari Kavu ya Kwala ina uwezo wa kuhudumia takribani makontena 300,000 kwa mwaka, huku taarifa zikitaja kuwa uwezo wake wa kuhifadhi na kuhudumia makontena unahitaji kuendana na ongezeko la mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, takribani makontena 1,350 yaliyopo Bandari Kavu ya Kwala yanahitaji kuondolewa ili kuongeza nafasi ya kuhifadhi na kuwezesha bandari hiyo kuendelea kuhudumia mizigo inayoongezek


No comments:
Post a Comment