HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 28, 2026

MWANZA YAPATA PAMPU 164, WAKULIMA 2000 KUNUFAIKA


Zaidi ya wakulima 2000 mkoani Mwanza wanatarajiwa kunufaika na kilimo cha umwagiliaji mwaka mzima baada ya Serikali kuwagawia pampu za kisasa 164.


Wakulima hao ambao asilimia 70 ni vijana, wanatoka katika vikundi 125 vinavyotoka kwenye wilaya sita za mkoa wa Mwanza.


Akikabidhi pampu hizo leo Alhamisi kwa niaba ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amesema pampu hizo zitaongeza kasi ya uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa wakulima na kuchangia katika mapinduzi ya kilimo mkoani humo.


Amesisitiza kuwa ugawaji wa pampu hizo unapaswa kuenda sambamba na utoaji elimu kwa wakulima kutoka kwa maofisa ugani waliosambazwa katika kata na vijiji mkoani humo.


Aidha, amewaasa wakulima kutumia pampu hizo kwa lengo lililokusudiwa ili kuleta matokeo chanya katika shughuli zao za kilimo.


Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Tume ya Umwagiliaji mkoa wa Mwanza, Mhandisi Said Kambi amesema pampu hizo zilizogharimu jumla ya shilingi bilioni 1.1 zitagawanywa kwa vikundi 125 vya wakulima.


“Mkoa wa Mwanza una hekta 40,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini ni hekta 3,300 zimeendelezwa kwa ajili ya kilimo hicho. Hivyo ujio wa pampu hizi utasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao katika kipindi chote cha mwaka.


“Ili kulinda mazingira na kuzuia kilimo cha pembezoni mwa vyanzo vya maji, zimefungwa mipira yenye urefu wa zaidi ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji, mifereji au mabwawa,” amesema.


Kila pampu ina uwezo wa kusukuma mita za ujazo 80 hadi 100 za maji kwa saa, hatua inayoiwezesha kumwagilia hadi ekari 40 kwa siku, huku uwepo wa magurudumu ukiwezesha urahisi wa kuzihamisha.


Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Magu, Edward Kihamba mbali na kuishukuru serikali kwa kuwapatia pampu 47 katika wilaya hiyo, pia ameahidi kushirikiana na madiwani wenzake kuhakikisha maofisa ugani wanatoa elimu inayotakiwa katika matumizi ya pampu hizo.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad