MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepokea jumla ya mawazo 9,545 ya ubunifu kutoka kwa wananchi ikiwa ni awamu ya pili ya mpango wa mawazo ya ubunifu, katika mchakato wa uchambuzi na tathmini ya mawazo ili kuwapata washindi 1020.
Mwenyekiti wa Kamati Huru ya Tathmini ya Wazo Bunifu, Zawadia Nanyaro amesema hayo leo Agosti 28, 2026.
Zawadia ameeleza kuwa awamu ya kupokea mawazo hayo ilizinduliwa Aprili Mosi, 2026 na kufungwa Julai 31, 2026 huku jumla ya wananchi 13,096 wakijisajili katika Mfumo wa Usimamizi wa Mawazo ya Ubunifu, ambapo mawazo 9,545 yaliwasilishwa.
Ameongezea kuwa Idadi hiyo imeongezeka kwa takribani asilimia 68 ikilinganishwa na mawazo 5,681 yaliyowasilishwa katika Awamu ya Kwanza.
Amefafanua kuwa mchakato huo wa uchambuzi na tathmini unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2026.
"Katika mchakato huo, mawazo 1,020 yatakayofikia hatua ya tathmini ya kina yatapata fursa ya kushindania zawadi mbalimbali, ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 50, washindi wawili wa nafasi ya pili watapata shilingi milioni 30 kila mmoja, washindi wawili wa nafasi ya tatu watapata shilingi milioni 20 kila mmoja na washindi 15 wa nafasi ya nne watapata shilingi milioni 10 kila mmoja". Amesema.
Ameongeza kuwa mawazo 1,000 yatakayobakia yatazawadiwa Shilingi 100,000 kila moja, pamoja na kutambuliwa kwa kupatiwa Cheti cha Ushiriki.
Aidha, amesisitiza kuwa mpango huo haujajikita katika kutoa zawadi pekee, bali unalenga kubaini na kuendeleza mawazo yenye uwezo wa kutatua changamoto halisi na kuleta maboresho yanayoonekana katika usimamizi wa kodi, utoaji wa huduma na ufanisi wa Mamlaka.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment