HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 4, 2026

Marais sita wa Afrika Kukutana Dar kwa Mkutano wa Africa50

Na Mwandishi Wetu
 
MARAIS sita wa Afrika wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanatarajiwa kushiriki Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika utakaofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria ni Rais wa Angola, João Lourenço, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, Rais wa Kenya, Dkt. William Samoei Ruto na Rais wa Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali imekamilisha maandalizi yote ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa kimataifa unaotarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,200 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, wakiwemo viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, viongozi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Chalamila amesema mkutano huo ni miongoni mwa majukwaa makubwa zaidi ya mwaka 2026 yanayolenga kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), huku ukiipa Tanzania fursa ya kujitangaza kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu Afrika.

Amesema kupitia mkutano huo, Serikali itawasilisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na miundombinu ya TEHAMA, kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kimataifa na kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Chalamila amewahakikishia wananchi na wageni wote kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ushirikiano wa wizara mbalimbali, taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama na wadau wengine ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika katika mazingira salama, tulivu na yenye viwango vya kimataifa. Aliongeza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga kuhakikisha wageni wote wanapata huduma bora tangu wanapowasili hadi watakapoondoka nchini.

Aidha, amewataka wananchi kuwapokea wageni kwa ukarimu, kudumisha usafi wa mazingira na kuzingatia sheria na taratibu za nchi, huku akiwahimiza wafanyabiashara na watoa huduma kutumia fursa hiyo kutoa huduma bora, zenye weledi na uadilifu pamoja na kuepuka upandishaji wa bei usio halali ili kuendelea kuijengea Tanzania taswira nzuri mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Chalamila amesema Serikali inaamini mafanikio ya mkutano huo yataongeza fursa za uwekezaji, kukuza uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na kufungua ajira na fursa mpya za maendeleo kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad