HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 17, 2026

YAS YAENZI URITHI WA MKAPA KWA KUWEKEZA TEKNOLOJIA KATIKA HUDUMA ZA AFYA

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Yas Tanzania imesema itaendelea kuenzi urithi wa Hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, kwa kuwekeza katika teknolojia za kidijitali na kuimarisha ushirikiano unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha urithi wa Hayati Mkapa, mwakilishi wa Yas Afisa Mkuu wa fedha Innocent Rwetabura alisema kiongozi huyo aliamini kuwa nguvu ya taifa hupimwa kwa ustawi wa wananchi wake, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga taasisi imara, mifumo endelevu na ushirikiano unaochochea maendeleo ya kizazi hadi kizazi.

Retabura alisema wakati Tanzania ikielekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, teknolojia imepewa nafasi muhimu katika kuimarisha sekta ya afya kupitia mifumo ya taarifa za afya, huduma za afya kidijitali na matumizi ya takwimu sahihi katika kufanya maamuzi.

Alieleza kuwa pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya afya, teknolojia sasa imekuwa nguzo muhimu katika kubadilisha namna huduma zinavyotolewa, ikiwemo tiba kwa njia ya mtandao (telemedicine), uchunguzi wa magonjwa kwa njia za kidijitali, mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya na huduma za dharura zinazowafikia wananchi kwa haraka.

Kwa mujibu wa Yas, mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji mkubwa wa kampuni katika sekta ya mawasiliano, ambapo katika kipindi cha miaka minne iliyopita imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kupanua upatikanaji wa teknolojia za 4G na 5G nchini kote.

Aidha, kampuni hiyo ilieleza kuwa maendeleo ya teknolojia yamefungua fursa kwa vijana wabunifu, wahandisi na wajasiriamali wa kijamii kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali za afya kupitia ubunifu wa kidijitali.

"Hayati Rais Mkapa aliwahi kusema kuwa mustakabali wa nchi uko mikononi mwa vijana. Leo tunashuhudia kauli hiyo ikitimia kupitia matumizi ya teknolojia ambayo yanawapa vijana uwezo wa kubuni suluhisho za kuboresha huduma za afya," alisema.

Yas pia ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ikisema ndiyo msingi wa kuharakisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kampuni hiyo ilitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali na wadau mbalimbali, ikiwemo mradi wa usajili wa vizazi kupitia RITA na UNICEF uliotumia teknolojia ya simu kuwezesha watoto chini ya miaka mitano kupata vyeti vya kuzaliwa kwa njia ya SMS, ambapo zaidi ya watoto milioni 13 wamesajiliwa.

Pia ilieleza kuwa imeshirikiana na Hospitali ya CCBRT katika matibabu ya watoto wenye tatizo la miguu ya kupinda (clubfoot), sambamba na kuendesha huduma za bure za uchunguzi na matibabu ya macho nchini Tanzania Bara na Zanzibar, ambazo hadi sasa zimewanufaisha zaidi ya Watanzania 23,000.

Katika hatua nyingine, Yas ilitangaza kuwa ipo katika mazungumzo na Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa kimkakati utakaotekeleza miradi endelevu ya afya na maendeleo kwa wanawake, watoto na vijana nchini.

Kampuni hiyo ilisisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika suluhisho bunifu za teknolojia ili kuimarisha mifumo ya afya, kupanua upatikanaji wa huduma bora na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya kuuenzi urithi wa Hayati Rais Benjamin William Mkapa.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad