HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 22, 2026

Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba Kuongoza Washiriki 13,000 NBC Dodoma Marathon.

· RC Dodoma awasihi madereva kutumia ‘ring road’ kuepusha foleni, kuhakikisha usalama wa washiriki.


Dodoma, Julai 22, 2026: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.) anatarajiwa kuongoza washiriki zaidi ya 13,000 wanaotarajiwa kushiriki mbio za NBC Dodoma Marathon zinazotarajiwa kufanyika Julai 26 katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, huku wito ukitolewa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri kutumia barabara mpya ya mzunguko ‘ring road’ ili kukwepa msongamano wa magari katika ya jiji hilo siku ya tukio hilo

Akizungumza wakati akipokea jezi maalum ya mbio hizo kutoka kwa waandaaji wa mbio hizo, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa maandalizi ya msimu wa saba wa mbio hizo alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa mkoa huo hususani wanaotumia vyombo vya usafiri kuangalia namna ya kukwepa kutumia barabara zinazohusishwa na mbio hizo hasa zilizopo katikati ya jiji hilo huku wale wanaotoka mikoa wakishauriwa kutumia Barabara mpya ya mzunguko ‘ring road’.

"Zaidi, nitoe wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kandokando ya barabara kuwashangilia na kuwapa hamasa washiriki wa mbio hizi. Kwa wale ambao hawatakuwa na ulazima wa kutumia magari yao siku hiyo, ni vyema wakaepuka kuyaingiza barabarani ili kupunguza msongamano wa magari na kuhakikisha usalama wa washiriki pamoja na watumiaji wengine wa barabara," alisisitiza

Hafla fupi ya kukabidhi jezi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Mkoa huo imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ikiwahusisha pia maofisa waandamizi kutoka ofisi hiyo, akiwemo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Mwajabu Nyamkumora, maofisa wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma, Bw. Godwin Semunyu, pamoja na wawakilishi wa wadhamini wa mbio hizo kutoka GSM Group na Vodacom Tanzania.

Bi. Senyamule, pamoja na kuwapongeza waandaaji wa mbio hizo, alieleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanyika, kuhusiana na mbio hizo zinazotarajiwa kuhusisha washiriki 13,000. Kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo, washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake watajishindia fedha taslimu za Shilingi milioni 11.5 kila mmoja, pamoja na nafasi ya kujinyakulia bonasi ya Shilingi milioni 5 endapo watafanikiwa kuvunja rekodi ya mshindi wa mwaka jana.

"Kukamilika kwa maandalizi ya mbio hizi kwa viwango vya kimataifa kunadhihirisha hadhi ya mbio hizi na nafasi ya Jiji la Dodoma kama Makao Makuu ya nchi. Zaidi ya hayo, kama Mkoa tunavutiwa na ajenda tatu muhimu za mbio hizi ambazo ni kukusanya fedha zitakazosaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua, kusaidia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, pamoja na kuimarisha mfuko wa huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya ugonjwa wa selimundu (sickle cell)," alisema.

Kwa mujibu wa Bi. Senyamule, kwa kipindi cha miaka saba ambayo mbio hizo zimekuwa zikifanyika mkoani Dodoma, zimeendelea kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo kuongeza mzunguko wa fedha kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za chakula, vinywaji, mavazi na malazi, kufuatia ujio wa takribani watu 20,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kushiriki na kushuhudia mbio hizo.

"Nitoe wito kwa wananchi wa Jiji la Dodoma, hususan wafanyabiashara,bodaboda, mama lishe, wadau wa utalii kuchangamkia fursa mbalimbali zitokanazo na ongezeko hili la wageni. Mbali na washiriki 13,000 waliothibitisha kushiriki, tunatarajia pia kuwapokea maelfu ya watu wengine watakaoambatana nao," alisema Bi. Senyamule.

Aliongeza kuwa amevutiwa pia na matukio mbalimbali yanayoambatana na mbio hizo, ikiwemo tamasha la Dodoma Wine Festival, linalolenga kutangaza soko la mvinyo na zabibu za Mkoa wa Dodoma, pamoja na tukio la NBC Dodoma Marathon Expo, linalolenga kuwaunganisha wafanyabiashara wa Mkoa huo na wateja kutoka maeneo mbalimbali.

Aidha, Bi. Senyamule aliwahimiza washiriki wa mbio hizo kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani Dodoma, ikiwemo kujionea utamaduni wa Wagogo kupitia ngoma za asili, sambamba na kutembelea mashamba ya zabibu ambayo yameifanya Dodoma kuwa kitovu cha kilimo cha zao hilo Afrika Mashariki.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, Bw. Godwin Semunyu, alitoa wito kwa wa kazi wa jiji la Dodoma hususani wanaotumia usafiri wa magarisema maandalizi yote ya mbio hizo yamekamilika na tayari washiriki wa mbio za kilomita 5, 10, 21 na 42 wanaendelea kuwasili jijini Dodoma kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo.

"Ili kuongeza mchango wa mbio hizi katika kukuza uchumi na burudani, tumeandaa matukio mbalimbali, ikiwemo tamasha la kuonja mvinyo (Dodoma Wine Festival) litakalofanyika Julai 24 hapa Dodoma, NBC Dodoma Marathon Expo litakalofanyika Julai 25, pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Marioo. Lengo letu ni kuongeza mzunguko wa fedha na kuhakikisha wenyeji wa Jiji la Dodoma wananufaika zaidi kupitia tukio hili," alisema Bw. Semunyu.

Zaidi, Bw. Semunyu aliwashukuru wadau na wadhamini mbalimbali wa NBC Dodoma Marathon kwa ushirikiano wao mkubwa uliochangia kufanikisha maandalizi ya msimu wa saba wa mbio hizo.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule (katikati) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa waandaaji na wadhamini wa mbio za NBC Dodoma Marathon ikiwa ni ishara ya kukamilisha maandalizi ya mbio pamoja na kumkaribisha rasmi mkuu wa mkoa huyo kwenye mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu (kulia), Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Mwajabu Nyamkumora (wa pili kulia) Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji Vodacom Tanzania, Bw Joseph Sayi (kushoto) na Meneja Masoko wa GSM Group Bi Neema Loth. Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika mapema leo kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa Dodoma.



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule (katikati) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa waandaaji wa mbio za NBC Dodoma Marathon ikiwa ni ishara ya kukamilisha maandalizi ya mbio pamoja na kumkaribisha rasmi mkuu wa mkoa huyo kwenye mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu (kulia), Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Mwajabu Nyamkumora (wa tatu kulia) pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule akionyesha sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa waandaaji wa mbio za NBC Dodoma Marathon ikiwa ni ishara ya kukamilisha maandalizi ya mbio pamoja na kumkaribisha rasmi mkuu wa mkoa huyo kwenye mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad