Na Mwandishi Wetu,Korea
TANZANIA imeendelea kuonesha uwezo wake katika jukwaa la kimataifa la UNESCO baada ya Bi. Rose Kinabo kuiwakilisha nchi katika Jukwaa la Vijana Wataalamu wa Urithi wa Dunia 2026, linalofanyika sambamba na Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia jijini Busan, Jamhuri ya Korea.
Katika kuonesha kutambua mchango huo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UNESCO, Mheshimiwa Saidi Yakubu, amekutana na Bi. Kinabo na kumpongeza kwa kuiwakilisha Tanzania kwa weledi na umahiri, baada ya kuchaguliwa kupitia mchakato wa ushindani mkubwa uliowashirikisha vijana kutoka mataifa 29 duniani.
Mheshimiwa Balozi Yakubu alisema mafanikio hayo yanaendelea kuthibitisha kuwa Tanzania ina hazina ya wataalamu vijana wenye uwezo wa kushiriki na kuchangia mijadala ya kimataifa kuhusu uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya Urithi wa Dunia.
Bi. Kinabo, ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtaalamu wa usimamizi wa urithi kwa kushirikisha jamii, aliwasilisha uzoefu wa Tanzania kuhusu usimamizi shirikishi wa maeneo ya Urithi wa Dunia pamoja na mchango wa taasisi za elimu katika kulinda na kuendeleza urithi huo. Uwasilishaji wake uliendana na kaulimbiu ya jukwaa la mwaka huu isemayo, “World Heritage, Communities and Education: Empowering Youth as Agents of Change.”
Mheshimiwa Balozi Yakubu alibainisha kuwa ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya vijana ya UNESCO unaimarisha sauti ya taifa katika masuala ya urithi wa dunia na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaalamu, utafiti, ubunifu na kujengeana uwezo kati ya wataalamu wa Tanzania na wenzao kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa, akieleza kuwa vijana ni nguvu muhimu katika kulinda urithi wa dunia na kuendeleza ajenda ya maendeleo endelevu kupitia elimu, utamaduni na ubunifu.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Balozi Yakubu aliambatana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia.
Ushiriki wa Bi. Rose Kinabo umechangia katika maandalizi ya Azimio la Vijana la UNESCO kuhusu Urithi wa Dunia, litakalowasilishwa rasmi mbele ya Kamati ya Urithi wa Dunia. Mafanikio hayo yanaendelea kuitangaza Tanzania kama nchi inayowekeza katika vijana, maarifa na ushirikishwaji wa jamii kama nguzo muhimu za kulinda na kuendeleza Urithi wa Dunia kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

.jpeg)

No comments:
Post a Comment