Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu usajili wa vyuo na kozi zinazotolewa kabla ya kuwaandikisha watoto wao, ili kuepusha hasara inayotokana na kusomea kozi zisizotambuliwa na Baraza.
Hayo ameyasema Afisa Uthibiti Ubora Mkuu wa NACTVET, Bi. Deborah Ngalemwa, alipokuwa akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Baraza hilo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Bi. Deborah amesema NACTVET imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa vijana wanaomaliza masomo yao katika baadhi ya vyuo, moja ya malalamiko hayo ikiwa ni pamoja na kutotambulika kwa vyuo na kozi walizosoma. Vijana wengi wamekutana na changamoto hii pale walipotaka kuendelea na masomo au wanapotafuta ajira.
Alieleza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya vyuo kuwaandikisha wanafunzi katika kozi ambazo hawana sifa za kujiunga nazo kulingana na matokeo ya mtihani wa Kidato cha nne, jambo ambalo huwasababishia matatizo wanapohitaji kutambuliwa na mamlaka zingine hasa zile za kitaaluma baada ya kuhitimu.
Aidha, alisema zipo pia kesi za wanafunzi wanaopelekwa kusoma katika vyuo vya nje ya nchi, lakini wanaporejea Tanzania wanashindwa kutambuliwa kwa sababu vyuo walivyosoma havitambuliwi au programu walizosoma hazikukidhi vigezo vilivyowekwa na Baraza.
Bi. Deborah aliwasihi wazazi, walezi na wanafunzi kufika NACTVET au kuwasiliana na Baraza hilo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano kabla ya kufanya uamuzi wa kujiunga na chuo chochote, ili kuthibitisha usajili wa Chuo pamoja na uhalali wa kozi wanazokusudia kusoma.
"Baraza limekuwa likipokea malalamiko kutoka kwa vijana wanaoambiwa vyuo walivyosoma havina sifa, ilhali wao na wazazi walikuwa tayari wamegharimia masomo, hali ambayo husababisha usumbufu na hasara kubwa kwa jamii ambayo ingeweza kuepukika kwa kupata ushauri mapema," alisema Bi. Deborah.
Aliongeza kuwa ushauri wa mapema kutoka NACTVET utawasaidia wazazi na wanafunzi kufanya maamuzi sahihi, kulinda uwekezaji wao katika elimu na kuhakikisha wahitimu wanapata sifa zinazotambulika katika soko la ajira na kwa maendeleo ya taaluma zao.
Baraza linaendelea kutoa Elimu kwa jamii kuhusu Umuhimu wa kujua uhalali wa Chuo na kozi kabla kuanza masomo kupitia kampeni zake mbalimbali zinazopatikana kwenye mitandao ya kijamii.


No comments:
Post a Comment