Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania, Bw. Bui Van Thang, leo ametembelea banda la Halotel katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), ambapo alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali za kisasa na suluhisho za kidijitali zinazotolewa na Halotel kwa Watanzania.
Katika ziara hiyo, Bw. Bui Van Thang aliambatana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania, Bi. Tran Thi Thuy Dung, huku wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara wa Halotel Tanzania, Bw. Abdallah Salum, ambaye aliongoza ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya maonesho na mabanda ya kampuni.
Katika banda la Halotel, viongozi hao walijionea huduma zinazowaunganisha wateja na teknolojia za kisasa, zikiwemo huduma za 5G, Halotel Fibre (intaneti ya majumbani), HaloPesa pamoja na huduma nyingine bunifu za kidijitali zinazolenga kurahisisha maisha ya Watanzania.
Ziara hiyo pia ililenga kuimarisha ukaribu kati ya kampuni, wafanyakazi na wateja, ambapo Mkurugenzi Mkuu alipata nafasi ya kuzungumza na timu ya Halotel inayohudumia wageni na wateja katika banda hilo. Aliwapongeza wafanyakazi kwa juhudi zao za kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na uzoefu mzuri wakati wa maonesho hayo.
Aidha, Bw. Bui Van Thang alikutana na baadhi ya wateja waliotembelea banda la Halotel na kushirikiana na timu ya watoa huduma kuwahudumia wateja, huku akishuhudia namna huduma za kampuni zinavyoendelea kurahisisha mawasiliano, biashara na shughuli mbalimbali za kila siku kwa Watanzania.
Akizungumzia ushiriki wa Halotel katika Sabasaba 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Halotel Tanzania amesisitiza dhamira ya kampuni ya kuendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuwapatia wateja huduma zenye ubora, uhakika na zinazokidhi mahitaji ya wakati huu wa mabadiliko ya kidijitali.
Kwa upande wake meneja masoko, Bi. Aidat Lwiza amewakaribisha Watanzania wote kuendelea kutembelea banda la Halotel katika Viwanja vya Sabasaba ili kujionea kwa karibu huduma mbalimbali zinazotolewa na Halotel.
Amesema kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wateja kupata taarifa zaidi kuhusu huduma za Halotel, kuzungumza na wataalamu wa kampuni, kujifunza kuhusu teknolojia mpya pamoja na kunufaika na ofa maalum zilizotayarishwa kwa kipindi hiki cha maonesho.
"Tunawakaribisha Watanzania wote kuendelea kututembelea katika banda letu la Halotel Sabasaba 2026. Wateja wetu watapata nafasi ya kujionea huduma zetu, kupata majibu ya maswali yao na kushiriki katika fursa mbalimbali tulizoandaa kwa ajili yao," alisema Bi. Aidat Lwiza.
Maonesho ya Sabasaba 2026 yanaendelea hadi Julai 13, 2026, na Halotel inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kushiriki katika maonesho hayo na kujionea namna teknolojia inavyoendelea kubadilisha maisha ya Watanzania.
Halotel – Teknolojia kutoka Moyoni.
#Halotel #HaloPesa #Sabasaba2026 #TeknolojiaKutokaMoyoni









No comments:
Post a Comment