Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Asha-Rose Migiro, amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Christine Grau, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Lumumba, Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamefanyika jana Juni 30,2026, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kumuaga Balozi Grau anayehitimisha kipindi chake cha uwakilishi nchini Tanzania. Viongozi hao walitathmini ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na kujadili namna ya kuuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu umuhimu wa kuimarisha misingi ya utawala bora, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa kama nguzo ya maendeleo endelevu ya Taifa. Katika muktadha huo, CCM ilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kujenga Taifa linaloongozwa kwa misingi ya haki, uwajibikaji na utulivu wa kisiasa.
Pia, ilitambua changamoto zilizojitokeza nchini katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu uliopita na umuhimu wa hatua ambazo Serikali inaendelea kuzichukua katika kuimarisha imani ya wananchi, ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi, Tume ya Upelelezi wa Jinai na hatua nyingine za kisheria zinazolenga kuhakikisha ukweli, uwajibikaji na haki vinaendelea kutawala katika kulinda amani na mshikamano wa Taifa.
Aidha, ilielezwa kuwa ajenda ya kuendelea kuimarisha demokrasia nchini, ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya ambao umeainishwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, inabaki kuwa sehemu muhimu ya maono ya muda mrefu ya kuimarisha utawala bora na mshikamano wa Taifa.
Viongozi hao pia walitambua nafasi ya vijana katika mustakabali wa maendeleo ya Tanzania na umuhimu wa kuhakikisha kizazi hicho kinaendelea kuwa sehemu ya safari ya Taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ujenzi wa uchumi wenye ushindani na maendeleo jumuishi.
CCM inathamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na inaamini kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarika kwa kuzingatia misingi ya kuheshimiana, maslahi ya pamoja na dhamira ya pamoja ya kuendeleza maendeleo endelevu ya Tanzania.








No comments:
Post a Comment