HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 2, 2026

HALOTEL NA SAMSUNG ELECTRONICS YAZINDUA USHIRIKIANO YA HUDUMA YA MKOPO WA SIMU KWA VIFURUSHI KWENYE MAONESHO YA SABASABA 2026

Kampuni ya Halotel Tanzania na Samsung Electronics leo imezindua rasmi huduma ya kibunifu ya mikopo ya simu janja iliyoambatana na promoshen ya bando kutoka Halotel, kwa lengo la kumwezesha kila Mtanzania kumiliki simu janja kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Uzinduzi huo umefanyika katika Banda la Halotel kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba).

Ushirikiano huu unaashiria hatua kubwa katika kuingia Ulimwengu wa kidijitali kwa kuwawezesha wateja kupata simu janja za Samsung kupitia njia mbalimbali za malipo, huku wakifurahia vifurushi vya Halotel vilivyoundwa kwa ajili ya mteja.

Wakati Tanzania ikiendelea kupokea mabadiliko ya kidijitali katika sekta mbalimbali, upatikanaji wa simu janja ni jambo la msingi, na kwa njia hiyo Halotel inaingia kati ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anajumuishwa katika ulimwengu wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa sherehe za uzinduzi huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania, Madam Tran Thi Thuy Dung, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kutoa suluhisho za kibunifu zinazopanua ufikiaji wa kidijitali na kuboresha maisha ya kila siku ya wateja.

"Sisi Halotel tunaamini kwamba kila mtu anapaswa kupata fursa ya kufurahia faida za mawasiliano ya kidijitali. Kupitia ushirikiano huu na Samsung Electronics, tunafanya simu janja zenye ubora kuwa za bei nafuu zaidi na zinazofikika kwa Watanzania, hasa kizazi cha vijana, huku tukihakikisha wanafurahia mawasiliano ya kuaminika na kupata promoshen vya mabando kutoka Halotel. Mpango huu unaonyesha dhamira yetu ya kuziwezesha jamii na kuunga mkono mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania," alisema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania.

Meneja wa Biashara wa Ofisi ya Samsung Electronics nchini Tanzania, Bw. Daesong Ra, alisema ushirikiano huo unaendana na mpango wa Samsung wa kupanua ufikiaji wa teknolojia na kusaidia uchumi wa kidijitali unaokua nchini Tanzania.

"Samsung inaamini kuwa teknolojia inapaswa kuwafikia kila mtu. Kwa kushirikiana na Halotel, tunatengeneza njia rahisi kwa wateja kupata vifaa halisi vya Samsung kupitia mikopo inayofaa, huku wakifaidika na suluhisho za mawasiliano kwa bei nafuu zinazoboresha uzoefu wao wa kidijitali. Pamoja, tunawasaidia Watanzania wengi zaidi kupata fursa za kidijitali," alisema.

Huduma hiyo mpya ya mkopo wa simu janja iliyozinduliwa inaruhusu wateja wanaokidhi vigezo kupata simu janja za Samsung kupitia mipango ya malipo ya awamu, ikisindikizwa na ofa za kipekee za vifurushi vya Halotel. Mpango huu unatarajiwa kuongeza matumizi ya simu janja miongoni mwa wanafunzi, wataalamu vijana, wajasiriamali, na familia kote nchini.

Wageni watakaotembelea duka lolote la Halotel watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu vifurushi hivi vya mikopo, kuona aina mbalimbali za vifaa vya Samsung vinavyopatikana, kupata msaada kutoka kwa wawakilishi wa Halotel na Samsung, na kupata ofa mbalimbali za promosheni ambazo Halotel imewaandalia wateja wote.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad