Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) umetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kutokomeza mazalia ya mbu katika kata 13 zenye jumla ya mitaa 78 ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita. Mradi huo unahusisha unyunyiziaji wa viuatilifu kwenye mazalia ya mbu, ukiwa na lengo la kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika manispaa hiyo.
Lengo la utekelezaji wa mradi huo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Halmashauri ya Manispaa ya Geita inafikia kiwango cha kutokomeza maambukizi ya malaria. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2025 jumla ya wagonjwa 10,845 waligundulika kuwa na ugonjwa wa malaria katika manispaa hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa GGML, Dkt. Kiva Mvungi, amesema kampuni hiyo imejipanga kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya malaria kutokana na athari kubwa za ugonjwa huo kwa wananchi wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza GGML kwa kufadhili mradi huo na kuomba kampuni hiyo kuangalia uwezekano wa kuupanua hadi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili wananchi wa maeneo hayo pia wanufaike na jitihada za kutokomeza malaria.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha azma ya kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030 na kuboresha afya pamoja na ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Geita.

.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment