BODI ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Prof. Joseph Msambichaka, imefanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kujionea utekelezaji wa usimamizi wa matumizi salama ya mionzi katika vifaa vya ukaguzi wa mizigo vinavyotumia teknolojia ya skana.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Msambichaka amesema Bodi imeridhishwa na kiwango cha uzingatiaji wa usalama wa mionzi pamoja na ufanisi wa matumizi ya skana katika ukaguzi wa makasha na mizigo. Amesema TAEC ina jukumu la kusimamia matumizi salama ya vifaa vinavyotumia mionzi kupitia utoaji wa leseni, ukaguzi wa mara kwa mara na mafunzo kwa watumiaji wa vifaa hivyo, ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi, madereva na wananchi kwa ujumla.
“Tumekuja kujionea kazi inayofanywa na TAEC katika kusimamia matumizi salama ya mionzi kwenye skana zinazotumika bandarini. Tumejiridhisha kuwa mazingira ya kazi ni salama kwa wafanyakazi, madereva na wananchi kwa ujumla,”amesema
amesema Prof. Msambichaka. Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia ya skana yameongeza ufanisi wa huduma bandarini kwa kupunguza muda wa ukaguzi wa makasha, kuimarisha usalama wa biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Usalama wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Dkt. Jumanne Fhika, amesema Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inatumia mashine 11 za skana ambazo zimeongeza kasi na ufanisi wa ukaguzi wa mizigo, kupunguza muda wa kuhudumia makasha na kuchangia ongezeko la mapato ya Serikali. Katika kuendelea na ziara hiyo, wajumbe wa Bodi ya TAEC walitembelea eneo la ukaguzi wa mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), ambapo walijionea namna TAEC inavyosimamia na kudhibiti matumizi ya vifaa vya mionzi vinavyotumika kukagua mizigo inayoingia na kutoka nchini. Ziara hiyo ililenga kujiridhisha kuwa matumizi ya teknolojia ya mionzi katika ukaguzi wa mizigo yanafanyika kwa kuzingatia viwango vya usalama ili kulinda wananchi, wafanyakazi na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mionzi.
Aidha, Bodi hiyo ilitembelea Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Mionzi na Uchafuzi wa Anga, kinachosimamia utekelezaji wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia (Comprehensive Nuclear-Test-Ban Treaty Organization – CTBTO).
Akitoa maelezo katika kituo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza kikamilifu wajibu wake wa kimataifa kwa kushiriki katika utekelezaji wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia, ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizouridhia mkataba huo.
Prof. Najat amesema kituo hicho kina jukumu muhimu la kufuatilia na kupima viashiria vya mionzi na uchafuzi wa anga, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa taifa, kulinda mazingira na kutekeleza wajibu wa Tanzania katika mfumo wa kimataifa wa ufuatiliaji wa majaribio ya nyuklia. Ziara hiyo imeiwezesha Bodi ya TAEC kujionea kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Tume katika maeneo muhimu ya kimkakati, yakiwemo usimamizi wa matumizi salama ya mionzi, ulinzi wa wananchi na mazingira, pamoja na matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kuimarisha usalama na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.



.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment