Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewataka waajiri nchini kutumia kikamilifu fursa ya msamaha wa tozo uliotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kulipa madeni ya michango ya wafanyakazi, akisisitiza kuwa hatua hiyo itapunguza gharama za uendeshaji, kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesema msamaha huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kusikiliza changamoto za waajiri ili kuongeza tija katika sekta binafsi na sekta ya ajira kwa ujumla.
Waziri Sangu alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa 67 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ambapo pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya NSSF na ATE, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano, kubadilishana taarifa na uzoefu, pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kwa manufaa ya waajiri, wafanyakazi na taifa.
Waziri Sangu alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara unaoendelea kuimarisha uchumi na kuboresha mazingira ya kazi nchini, akibainisha kuwa sekta ya ajira imeendelea kukua kutokana na sera madhubuti na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema msamaha huo ulioanza kutekelezwa Juni 1, 2026 hadi Desemba 31, 2026 unalenga kutoa unafuu kwa waajiri, kupunguza gharama na kuwawezesha zaidi katika uzalishaji.
Bw. Mshomba aliongeza kuwa ushirikiano kati ya NSSF na ATE utaimarisha utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa mifumo ya kinga ya kijamii kwa waajiri na wafanyakazi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba-Doran, ameeleza kupongeza uamuzi wa NSSF wa kutoa msamaha wa adhabu na tozo, akisema hatua hiyo ni muhimu kwa waajiri kwani inawapa nafasi ya kurekebisha na kutimiza wajibu wao wa kisheria bila kuathiri kwa kiasi kikubwa uendelevu wa biashara zao. Alibainisha kuwa msamaha huo unaakisi ushirikiano wenye tija kati ya Serikali na taasisi za hifadhi ya jamii katika kuimarisha utii wa sheria, kuongeza usajili na michango, pamoja na kulinda maslahi ya wafanyakazi.
“Tunawahimiza waajiri kuitumia ipasavyo fursa hii kurekebisha hali zao za utii wa michango bila kuchelewa,” alisema. Aliongeza kuwa ATE imeendelea kusambaza taarifa za msamaha huo kwa wanachama wake kupitia mifumo yake ya mawasiliano, sambamba na kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa waajiri ili kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo kwa manufaa ya uendelevu wa biashara na ustawi wa sekta ya ajira kwa ujumla.




.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment