Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewakamata wamiliki watatu wa mgodi wa uchimbaji madini wa Lupande Zabron Kisaba uliopo Kijiji cha Iparamasa, Halmashauri ya Wilaya ya Chato, kwa tuhuma za kuhujumu uchumi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia matumizi yasiyo halali ya nishati ya umeme.
Wanaotuhumiwa katika tukio hilo ni Masunga Mashauri, Lupande Kisaba na Lopa Pam. Inadaiwa kuwa walivuta umeme kwa njia isiyo halali kutoka kwenye mita kwa umbali unaozidi mita 120, pamoja na kutumia mita za umeme zilizosajiliwa kwa matumizi ya maeneo mengine tofauti na eneo la mgodi huo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Geita, Eleutherius Katemana, amesema operesheni maalum ya kubaini na kudhibiti wateja wanaohujumu nishati ya umeme imebaini ukiukwaji wa taratibu za matumizi ya umeme katika mgodi huo.
Katemana amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa wahusika walijiunganishia umeme kinyume cha utaratibu wa TANESCO, hali iliyosababisha shirika hilo kupata hasara ya mapato.
Kwa upande wake, mmoja wa wamiliki wa mgodi huo, Masunga Mashauri, amesema wanahitaji kupewa maelekezo ya namna sahihi ya kutekeleza taratibu za huduma ya umeme, akidai kuwa baadhi ya maafisa waliowahudumia walihusika katika kuwaunganishia huduma hiyo.
Naye mwekezaji mwingine katika mgodi huo, Lopa Pam, amesema hahusiki moja kwa moja na mifumo ya umeme iliyowekwa mgodini, akieleza kuwa jukumu la kufuata sheria na taratibu za nchi lilikuwa chini ya mwenye leseni ya shughuli za uchimbaji.
TANESCO Mkoa wa Geita imeeleza kuwa itaendelea na operesheni hiyo katika maeneo mbalimbali ya mkoa kwa lengo la kubaini na kuchukua hatua dhidi ya wote wanaohujumu miundombinu ya umeme na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Aidha, wananchi na wafanyabiashara wametakiwa kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya umeme ili kuepuka hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao.






No comments:
Post a Comment