HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 23, 2026

Serikali Yazindua Mradi wa Uhifadhi Bonde la Tanganyika

 



Na Mwandishi Wetu, Tabora
SERIKALI imezindua rasmi Mradi wa Uhifadhi wa Bioanuai, Usimamizi Endelevu wa Ardhi na Kuongeza Usalama wa Maji katika Bonde la Ziwa Tanganyika, hatua inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya bonde hilo.

Uzinduzi wa mradi huo ulifanywa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Ally Babu, ambaye alisema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha rasilimali za asili zinatumika kwa njia endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Babu alizitaka taasisi za umma, washirika wa maendeleo na wananchi kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mradi ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Alisema mradi huo utachangia kuimarisha uhifadhi wa bioanuai, matumizi bora ya ardhi na usalama wa maji, huku ukiwanufaisha wananchi wanaotegemea rasilimali za Bonde la Ziwa Tanganyika kwa shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Ni muhimu wadau wote tushirikiane kwa karibu ili kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo yaliyokusudiwa. Mafanikio yake yatachangia uhifadhi wa mazingira, kuimarisha usalama wa maji na kuboresha ustawi wa wananchi,” alisema Babu.

Aliongeza kuwa Serikali inatarajia kuona utekelezaji wa haraka wa shughuli za mradi huo ili manufaa yake yaanze kuonekana kwa wananchi na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika, Bona Mremi, alisema Bonde la Mto Malagarasi limepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhifadhi mfumo wa ikolojia wa Ziwa Tanganyika.

Alisema bonde hilo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 67,000 na wakazi wapatao milioni sita ni chanzo muhimu cha maji yanayoingia katika Ziwa Tanganyika, hivyo uhifadhi wake ni muhimu kwa mustakabali wa ziwa hilo.

Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa kuchochea uhifadhi wa mazingira, usalama wa maji na matumizi endelevu ya ardhi katika Bonde la Ziwa Tanganyika, huku ukilinda rasilimali muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad