DODOMA: Serikali imesema haijauza wala haijakabidhi rasilimali za misitu au maliasili za Tanzania kwa mataifa ya nje kupitia makubaliano ya biashara ya kaboni, ikisisitiza kuwa hatua zinazoendelea zinalenga kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa taifa huku zikilinda maslahi ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amekanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, akieleza kuwa taarifa zinazodai serikali imekabidhi maliasili kwa wawekezaji wa nje si za kweli na zinapotosha umma.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msingi wa kisheria na kiutawala wa kusimamia biashara ya kaboni ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na soko la kimataifa la biashara hiyo.
Kwa mujibu wa Mhe. Masauni, bajeti ya mwaka wa fedha wa sasa imetenga fedha kwa ajili ya kuanzisha mifumo ya usajili, ukaguzi na ufuatiliaji wa biashara ya kaboni. Alieleza kuwa mifumo hiyo itasaidia kudhibiti shughuli zote zinazohusiana na biashara hiyo na kuhakikisha mapato yanayostahili yanapatikana kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema serikali imeunda kamati ya wataalamu kutoka wizara mbalimbali ili kupitia fursa zilizopo katika sekta ya biashara ya kaboni na kupendekeza namna bora ya kuongeza manufaa kwa taifa bila kuhatarisha uhifadhi wa mazingira na rasilimali za asili.
Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na mataifa mbalimbali, Mhe. Masauni alisema makubaliano yaliyofikiwa na nchi kama Oman, Singapore, Japan na Korea yanahusu ushirikiano wa kiuchumi na kufungua masoko ya biashara, badala ya kuhamisha umiliki wa rasilimali za Tanzania.
Alisisitiza kuwa hakuna makubaliano yanayoruhusu taifa jingine kumiliki au kusimamia maliasili za Tanzania, akibainisha kuwa rasilimali zote za nchi zitaendelea kulindwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Masauni aliwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu biashara ya kaboni na kufuatilia taarifa rasmi za serikali, akieleza kuwa hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na fursa za soko la kimataifa huku ikihifadhi mazingira na kuongeza mapato ya taifa.


No comments:
Post a Comment