Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa kikanda wa Pen-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026) unaofanyika kwa siku gatu kuanzia leo Juni 23, 2026 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC, jijini Dar es Salaam.
Na Karama Kenyunko,Michuzi TV
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hakuna maisha ya mwafrika yanayopaswa kupotea kwa sababu huduma za afya zilikuwa mbali, ghali au zilichelewa kupatikana.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus Afrika 2026, Mchengerwa alisema ukweli unaotia wasiwasi ni kwamba vifo vingi vya mapema vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, nyingi zikiwa barani Afrika.
“Hili si suala la kitabibu pekee; ni suala la usawa. Ni swali la kama mahali alipozaliwa mtu, anapoishi au kipato chake kinaweza kuamua kama atapata huduma bora kwa wakati,” alisema.
Alisema Tanzania imeamua kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuhakikisha asilimia 80 ya jamii zinafikia huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka makazi yao.
Mchengerwa alisema mkakati wa PEN-Plus umeendelea kuwa moja ya ubunifu muhimu zaidi barani Afrika kwa kuwezesha huduma za magonjwa sugu na magonjwa yasiyoambukiza kutolewa katika hospitali za wilaya na vituo vya afya badala ya kutegemea hospitali za rufaa pekee.
“Huduma maalumu hazipaswi kubaki katika hospitali za rufaa zilizoko mbali wakati wagonjwa wanahitaji msaada endelevu karibu na jamii zao,” alisema.
Alibainisha kupitia ushirikiano wa serikali na wadau mbalimbali pamoja na Programu ya Samia Suluhu Outreach, huduma za PEN-Plus zinaendelea kupanuliwa nchini hususan katika maeneo ya vijijini na yaliyokuwa nyuma kimaendeleo.
Alizitaka nchi za Afrika kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya afya, kuimarisha tafiti na ubunifu, kuboresha upatikanaji wa dawa na teknolojia za afya pamoja na kujenga mifumo imara ya afya.
“Afya ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Taifa linalowekeza katika afya linawekeza katika nguvu kazi yake, watoto wake, wanawake wake, wazee wake, uzalishaji wake na mustakabali wake,” alisema.

.jpeg)


No comments:
Post a Comment